Rais Magufuli kukutana na Prince William

 Mwanamfalme William wa Uingereza anapangiwa kukutana na rais wa Tanzania Dkt John Magufuli wiki ijayo wakati wa ziara yake ya siku saba Afrika.

Anatarajiwa kuzuru pia Kenya na Namibia katika ziara hiyo ambayo si ya kikazi. Ziara hiyo itafanyika kuanzia 24 Septemba hadi 30 Septemba.

Lengo kuu la mwanamfalme huyo litakuwa kufuatilia juhudi za kukabiliana na ujangili na uhifadhi wa wanyama.

Atafanya ziara hiyo katika wadhifa wake kama rais wa mashirika yanayotetea uhifadhi wa wanyama ya United for Wildlife na Tusk Trust.

Amekuwa pia mlezi wa shirika la Royal African Society linalolenga kukuza uhusiano kati ya Afrika na Uingereza na hushiriki sana juhudi za kukabiliana na ujangili.

Akiwa ziarani Tanzania, Mtawala huyo wa Cambridge, atafanya mashauriano na Rais Magufuli kuhusu juhudi zinazopigwa na Tanzania katika kukabiliana na ujangili na ulanguzi wa wanyama pori kwa mujibu wa shirika la habari la Press Association.


from MPEKUZI

Comments