Lukuvi Amnyang'anya Hati ya Viwanja Mwekezaji

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Mendeleo ya Makazi, William Lukuvi  ameitaka kampuni ya Magarya engineering kurejesha haraka kwake hati ya umiliki wa viwanja vitano katika eneo la uwanja wa ndege wilayani Tarime ili eneo hilo liweze kukabidhiwa  kwa watu wengine kwaajili ya shughuli za maendeleo.

Agizo hilo amelitoa leo Septemba 18,2018 alipofika katika eneo hilo na wananchi kumuomba awasaidie ili waweze kumiliki viwanja hivyo na kufanya shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule ya msingi kwaajili ya wakazi wa eneo hilo.

Waziri Lukuvi alisema kutokana na mmiliki wa eneo hilo kushindwa kuliendeleza eneo lake japokuwa anamiliki hati kwa zaidi ya miaka 20 huku akishindwa kulipia kodi ya zaidi ya Sh40 milioni.

Amemtaka mmiliki wa kampuni hiyo aliyejulikana kwa Magarya Mwita Manko kuwasilisha hati hiyo kwake kabla hajaondoka wilayani Tarime leo na kuwaagiza viongozi wa halmashauri ya mji wa Tarime kuhakikisha mtu huyo anapatikana.

"Hatuwezi kumuangalia tu huyo mtu amepewa kiwanja zaidi ya miaka 20 bila kuliendeleza na hata kodi halipii halafu tunamuangalia tu ni lazima tuchukue hatua, " amesisitiza waziri huyo

Mwenyekiti wa mtaa wa Uwanja wa Ndege, Musa Mukunye amesema wameishi katika eneo hilo kwa muda mrefu na kwamba tayari wananchi wameanza ujenzi wa shule ya msingi kwaajili ya watoto wao lakini hivi karibuni mtu huyo alijitokeza na kuwazuia kufanya shughuli yoyote katika eneo hilo kwa madai kuwa eneo hilo  ni mali yake.

Alisema tayari wamejenga madarasa saba kwa ajili ya shule ya msingi kutokana na watoto wao kutembea umbali mrefu kwenda shule na kumuomba waziri huyo kuingilia kati ili waweze kuendelea na shughuli zao ikiwemo ujenzi wa shule hiyo.


from MPEKUZI

Comments