Hatima Ya Nondo Kujulikana Oktoba 2

Mahakama ya Hakimu Mfawidhi mkoa wa Iringa  imefunga kusikiliza ushahidi wa  shauri linalomkabili mwenyekiti wa mtandao wa wanafunzi Abdul Nondo baada ya kusikiliza mashahidi wawili wa upande wa utetezi, ambapo imepanga Oktoba 2 kutaja siku ya kutoa hukumu ya kesi hiyo.

Kabla ya kufunga ushahidi huo Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya mkoa Iringa Liad Chamshama amesikiliza mashahidi wawili wa upande wa utetezi ambapo shahidi wa kwanza ni  Abdul Nondo  na shahidi wa pili ni  Alphonce Lusako.

Akitoa ushahidi mbele ya Hakimu  jana Abdul Nondo akiongozwa na wakili wake Jebra Kambole, Nondo amedai kuwa alitekwa na watu wasiojulikana karibu na geti la chuo cha maji ubungo majira ya  saa tano Usiku, siku ya tarehe 6 Machi 2018, kwa kuvamiwa na kutupwa siti ya nyuma ndani ya gari.

Nondo amesema  watu hao walikuwa wakimhoji kwanini anatumiwa na wanasiasa kiasi cha kuvuruga amani na walimtuhumu kuwa anatumiwa na Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, Zitto Kabwe na Hellen Kijo Bisimba (aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu-LHRC) pamoja na kumshutumu kuwa yeye ni wakala wa Mange Kimambi katika kuandaa maandamano ya wanafunzi lakini amekana tuhuma hizo.

Kwa upande wake shahidi wa pili Alphoce Lusako ambaye ni kiongozi mwezake katika shirika la TSNP ameiambia  mahakama kuwa baada ya kupata taarifa kutoka  kwa Paul Kinabo kuwa amepokea ujumbe kwa njia ya simu  kutoka kwa Nondo kuwa yupo hatarini  na ndipo wakatoa taarifa kwa uongozi wa chuo na askari wasaidizi wa chuo na kupewa RB.

Mtuhumiwa Abdul Nondo alifikishwa  Mahakamani Machi 21, 2018 na kusomewa mashitaka yake ambayo yote aliyakana kuhusika nayo hivyo Oktoba 2 mwaka huu Mahakama itarejea tena kwa ajili ya kutaja siku ya hukumu.


from MPEKUZI

Comments