Fedha ya Zambia kuanza kutumika Tanzania

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga na mwenzake wa Benki Kuu ya Zambia, Dk. Denny Kalyalya, wanatarajia kutia saini makubaliano ya kuruhusu matumizi ya fedha za nchi mbili shilingi ya Tanzania na Kwacha ya Zambia ziweze kutumika katika nchi hizo mbili hasa katika eneo la mpakani la Tunduma na Nakonde.

Hatua hiyo sasa inakwenda kutoa fursa ya kiuchumi kwa kufanya biashara na uwekezaji katika miji ya mpakani ya Tunduma (Tanzania) na Nakonde (Zambia).

Makubaliano hayo yanatarajiwa kusainiwa kesho mkoani Songwe mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa huo, Brigedia Jenerali Nicodemas Mwangela na baada ya tukio hilo utafanyika mkutano wa hadhara katika eneo la Tunduma ambapo magavana hao watazunguza na wananchi wa pande zote mbili.

Taarifa iliyotolewa  na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ilieleza kwamba lengo la makubaliano hayo ni kuwezesha kupokelewa sarafu za nchi hizo mbili na taasisi rasmi za fedha ikiwa ni pamoja na mabenki ya biashara ya pande zote mbili bila kikwazo chochote.

“Nia ya hatua hii ni kurahisisha biashara kati ya nchi hizi mbili, kuondoa biashara holela ya fedha za kigeni mpakani na kuziwezesha serikali za Tanzania na Zambia kujipatia mapato stahiki ya kodi na tozo kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazofanyika katika miji hiyo.

“Benki Kuu za mataifa haya mawili rafiki, zimefikia hatua ya kusaini makubaliano hayo baada ya utafiti na majadiliano yaliyoanza tangu mwaka jana ambayo yalikuwa na lengo la kupambana na biashara holela ya fedha za kigeni na kuwawezesha wananchi wa pande zote kunufaika na shughuli za kiuchumi za mpakani,” ilieleza taarifa hiyo.

Makubaliano hayo yatasaidia kuleta ushindani wa haki kwa taasisi za fedha hasa kwa mabenki na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni katika biashara na kuziwezesha Benki Kuu za nchi zote mbili kusimamia ipasavyo ujazi wa fedha katika soko.

Kwa muda mrefu wananchi wa Tanzania na Zambia wamekuwa wakishirikiana katika nyanja mbalimbali kwa miaka mingi.

Ushirikiano huo uliimarishwa zaidi na viongozi waasisi wa mataifa haya, Rais Mstaafu wa Zambia Dk. Kenneth Kaunda na Hayati Mwalimu Julius Nyerere kwa kuanzisha reli ya pamoja ya Tazara , bomba la mafuta la Tazama, harakati za ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika pamoja na masuala mengine mengi ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Viongozi wa sasa wa serikali zote mbili Rais Dk. John Magufuli na Edgar Lungu wa Zambia wanaendelea kuimarisha ushirikiano huo.

Hatua za utiaji saini wa makubaliano hayo unatarajiwa kuongeza hamasa kwa wananchi na taasisi mbalimbali kufanya shughuli za kiuchumi ili kujiletea maendeleo na kuchangia maendeleo kwa nchi zote mbili.





from MPEKUZI

Comments