Breaking: CHADEMA Watangaza Kususia Chaguzi Zote

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetangaza kujiondoa Rasmi kushiriki chaguzi ndogo zote zilizotangazwa kufanyika hivi karibuni na chaguzi zozote zitakazofuata zinazosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa madai kwamba tume hiyo inafanya kazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mbowe amesema hayo leo Septemba 19, 2018 alipokuwa akiwasilisha uamuzi wa kamati ndogo ya Kamati Kuu ya Chadema iliyokutana jana kutafakari yaliyotokea kwenye chaguzi ndogo za ubunge za Ukonga, Monduli na kata 23 uliofanyika Jumapili iliyopita ya Septemba 16, 2018.

Mbowe amesema hujuma za uchaguzi huanza mapema katika hatua za kupata wagombea ambapo wakurugenzi wanatumika kubaka demokrasia ya nchi.

Amesema kwenye uchaguzi uliopita wakurugenzi walitumika kuhakikisha wagombea wa chama tawala wanapita bila kupingwa.

"Walikuwa wanafunga milango wanaondoka, muda ukiisha wanatangaza mgombea wa Chadema hakurudisha fomu hivyo wa CCM amepita bila kupingwa" amesema Mbowe.

“Kwa sasa tunakwenda kufanya mabadiliko ndani ya chama, tunakwenda kujijenga na hatuwezi kushiriki wakati tunaonewa na sheria hazifuatwi. Kwa sasa tunarudi nyuma,” ameongeza:

Amesema kumekuwa na tatizo kubwa la wasimamizi wa vituo vya kupigia kura kutotambulika mapema huku suala hilo likifanyika kwa makusudi maalumu.

Mbowe ambaye ni kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni amesema kwenye Jimbo la Ukonga kulikuwa na vituo feki 16 vyenye wapiga kura 700,000.

“Ukonga kulikuwa na vituo feki 16 vyenye wapiga kura zaidi ya 7,000 na viliandaliwa mahususi kwa ajili ya kuongeza kura za CCM. Tulipeleka malalamiko yetu NEC na kwa Msimamizi wa Uchaguzi, hakuna kilichofayika.

“Upole na ukimya wa vyama vya upinzani hauashirii uoga hata kidogo, yale mawazo ya wenzetu wa Chama Cha Mapinduzi kuamini wana dola na ndio wenye nguvu ni kujidanganya, hakuna jeshi linaloweza kuwa na nguvu kuwazidi raia wa Tanzania. "

Amesema kuna mambo ya kibatili yalifanyika kwenye uchaguzi wakitoa matamko na kutoa ahadi kwa wananchi wakati wa kampeni wakitumia magari ya Serikali.


from MPEKUZI

Comments