Serikali Yazifutia Kodi Taasisi Zinazotoa Huduma

Na. Hassan Maabuye, Wizara ya Ardhi
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amesema serikali imefuta kodi ya pango la ardhi katika majengo na maeneo yote ya taasisi ambazo zinatoa huduma katika jamii bila kufanya biashara na kuzalishi faida.

Waziri Lukuvi amesema hayo wakati alipofanya ziara ya utatuzi wa migogoro ya ardhi ya wakazi wa jiji la arusha ambapo ametoa agizo kwa maafisa wote wanaohusika na ukusanyaji wa kodi ya pango la ardhi kuziondoa katika orodha ya madeni taasisi binafsi, za dini, za serikali na mashirika yote ambayo hayazalishi faida.

Hata hivyo waziri Lukuvi amesema kwamba sheria hiyo imeanza kutekelezwa kuanzia tarehe 1 julai 2018 ambapo Serikali kupitia Bunge imeridhia kuondolewa kodi ya pango la ardhi taasisi za elimu, shule za msingi, sekondari, vyuo, vituo vya afya, hospitali, taasisi za umma na taasisi za dini kama misikiti na makanisa ambayo yalikuwa yanalipa kodi hiyo.

Pamoja na msamaha huo wa kodi Waziri Lukuvi amewaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri kote nchini kupima maneo yanayotoa huduma kwa jamii ili kuitambua mipaka ya shule, zahanati na maeneo mengine na kuzipatia hati miliki za ardhi zitakazo wawezesha kutambua mipaka ya maeneo hayo lakini taasisi hizo hazitalipa kodi tena.

“Yale maeneo ambayo yana hati ya pamoja wakati sehemu ya eneo inatumika kuzalisha faida basi maafisa ardhi watakokotoa eneo linalozalisha faida na wataliondoa lile eneo linalozalisha faida na kulitoza kodi, mfano eneo la Mlimani City ambalo linazaliosha faida katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam” amsema Mhe Lukuvi.

Aidha, katika hatua nyingine Waziri Lukuvi amesema kwamba kuanzia sasa vibali vya ujenzi vitakuwa vinatolewa kila wiki na vitakuwa vinatolewa na maafisa wa serikali waliopo wilayani ambao ni maafisa mipango miji, maafisa ardhi, wapimaji na wathamini ambao ni wataalamu.

“Kulikuwa na ucheleweshaji wa utoaji vibali vya ujenzi Mheshimiwa Rais ameshatoa maelekezo kwamba vibali vya ujenzi havitatolewa tena na kamati za madiwani kwasababu ilikuwa inachukua muda na walikuwa lazima walipwe posho, kwahiyo vibali vya ujenzi vitakuwa vinatoka kila wiki na vitatolewa na wataalamu wa serikali waliopo wilayani” amsema Mheshimiwa Lukuvi.

Amesema kwamba Serikali imeamua kubadili utaratibu huo ili kuwawezesha wananchi ambao walikuwa wana fedha ya kujenga maeneo yao lakini vibali vya ujenzi vilikuwa havitolewi kwa wakati, na kuna watu ambao walikuwa wanakaa mwaka mzima wakisubiri vibali vya ujenzi kitendo amabacho kilichangia ujenzi holela katika miji.

Mheshimiwa Lukuvi amesema serikali imeamua kuchukua hatua hizo ili kuondoa kero kwa wananchi ambao walikuwa wanapata tabu ya urasimu uliokuwepo hapo awali, kitu ambacho kilikuwa ni kikwazo katika kuleta maendeleo ya nchi yetu.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amesikiliza kero za migogoro ya ardhi ya wananchi zaidi ya 200 wa jiji la Arusha ambao walihudhuria katika mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Azimio la Arusha jijini hapo.


from MPEKUZI

Comments