Serikali Yasisitiza Wafungwa Kutumika Katika Shughuli Za Uzalishaji

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad  Masauni  amekabidhi mashine 10 za kufyatulia matofali kwa  jeshi la magereza la mkoa wa Lindi na kuwataka kuzitumia ipasavyo ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili ikiwemo makazi duni.

Mashine hizo ni sehemu ya ahadi aliyoitoa mwaka mmoja na nusu uliopita baada ya kufanya ziara katika mkoa wa Lindi.

Masauni alikabidhi mashine hizo  katika gereza la Lindi mjini  mkoani hapa na kuwataka jeshi la magereza kujipanga ipasavyo namna ya  kuzitumia ili ziwe na tija na manufaa kwao.

Alisema mwaka uliopita alifanya  ziara ya kukagua shughuli za magereza na kukutana na changamoto mbalimbali ikiwamo makazi duni ya nyumba za udongo hasa katika gereza la Lindi Mjini.

“Nawakabidhi mashine hizi leo, natarajia kuona mabadiliko yenye tija kutoka kwenu. Mkifanya vizuri nitawatafuta wadau wengine kwa ajili ya kuongeza mashine hizi,” alisema Masauni na kuongeza kuwa;

“Nataka gereza la Lindi Mjini liwe la mfano kwa magereza ya mkoa huu. Tumieni nguvu kazi ya wafungwa mlionao kwa ajili ya kuboresha makazi yenu,” alisema Masauni.

Alisema atalishangaa jeshi la magereza endapo hawatumii ipasavyo nguvu kazi ya wafungwa wakati wana changamoto mbalimbali zinazowakabili na njia za kuzitatua zipo wazi.

Hata hivyo, Masauni alisema ana matumaini makubwa na magereza katika kukabiliana na changamoto mbalimbali na watazitumia mashine kwa ufanisi ili wapate makazi bora kwa manufaa ya askari na maofisa wao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza ya Mkoa wa Lindi (RPO), Kamishna Msaidizi Mwandamizi , Rajab Nyange  alisema hali ya makazi ya askari wa jeshi hilo siyo nzuri hivyo alimshukuru Masauni kwa msaada wa mashine hizo za ujenzi.

Mkuu wa gereza la Lindi Mjini (SP), Emanuel Pagali alisema mashine hizo ni nzuri na zitawasaidia kwa utekelezaji wa majukumu yao ikiwamo kuboresha makazi ya maofisa na askari wa jeshi hilo


from MPEKUZI

Comments