Serikali Yaanza Kuandaa Kanauni Za Kutoa Vibali Vya Kuwinda Wanyamapori Kwa Ajili Ya Kitoweo

Na Lusungu Helela-morogoro
Serikali imesema inaandaa kanuni  zitakazoruhusu kufanyika uwindaji wa kiasili (Local Hunting)  kwenye maeneo ya wazi kwa ajili ya kitoweo ili wananchi waweze kunufaika moja kwa moja na Maliasili zao ili waone umuhimu wa kuhifadhi.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amesema hayo jana  wakati alipokuwa akizungumza na Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kikazi mkoani Morogoro kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali  zinazoikabili Maliasili, Malikale na Uendelezaji Utalii.

Amesema wawindaji hao watapewa vibali maalum  vitakavyowawezesha kuwinda kwa ajili ya kujipatia vitoweo vya  nyamapori na kutakuwa na maeneo maalum kwa ajili ya kuuzia vitoweo hivyo  kwa jamii.

Aidha, Ametaja aina za vitoweo vitakavyokuwa vinauzwa kwenye maeneo hayo  maalum  ikiwa pamoja na  nyama ya mamba, nyati,swala viboko na wengineo.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi za Taifa za Mikumi, Godwell Ole Meng'ataki amesema kama kutakuwa na utaratibu mzuri itaweza kusaidia kuongeza mapato kwa nchi.

Aliongeza kuwa utaratibu huo wa kuwa na sehemu maalum ya kuuzia vitoweo si mgeni kwa vile nchi kama Afrika Kusini wamekuwa wakifanya hivyo na pia wana  maeneo maalum kwa ajili ya kuuzia viteweo vya nyamapori.


from MPEKUZI

Comments