Rais Magufuli Apongeza Jimbo La Mbulu Kupata Askofu Mpya

RAIS John Magufuli amewapongeza wananchi wa wilaya za Mbulu, Babati na Hanang’ mkoani Manyara na Karatu mkoani Arusha zinazounda Jimbo la Mbulu kwa kumpata askofu wa tano wa Jimbo hilo Anthony Lagwen.

Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi ambaye alimwakilisha Rais Magufuli aliyasema hayo jana mjini Mbulu Mkoani Manyara, kwenye tukio la kusimikwa kwa askofu Lagwen.

Waziri kabudi alisema pamoja na kuwapongeza, kanisa katoliki limekuwa msaada mkubwa kwa serikali kwa kutoa huduma ya elimu, afya na maji hasa kwa watu wa kawaida.

Alisema jimbo la Mbulu linaloundwa tangu mwaka 1953 limekuwa mfano wa kuigwa katika kuhakikisha jamii ya eneo hilo inapata huduma za kiroho na kimwili.

“Tunapongeza kanisa katoliki jimbo la Mbulu kwa kutoa huduma za afya ikiwemo hospitali za misheni za Dareda na Bashnet wilayani Babati,” alisema.

Alipongeza jimbo hilo kumiliki kituo cha redio Habari Njema ambacho kwa namna moja au nyingine kinatoa huduma ya uinjilishaji na kuhabarisha jamii.

“Kituo hicho cha redio kiendelee kusisitiza amani kwani bila uwepo wa amani hakutawezekana kufanyika chochote,” alisema.

Alisema taasisi za dini kwa kiasi kikubwa zimechangia maendeleo mengi na ustawi wa jamii hivyo serikali itaendelea kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha jamii inasonga mbele.

Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es salaam, mwadhama Policarp Kardinali Pengo alisema japokuwa askofu Lagweni ni mzaliwa wa jimbo la Mbulu lakini atakumbana na changamoto zile zile wanazokumbana nazo maaskofu ambao wanaongoza majimbo ambayo hawajazaliwa.

“Mimi siwezi kuona Sumbawanga ndiyo bora zaidi kuliko sehemu ninayoongoza waumini hivyo nawe waongoze waamini kama inavyopaswa kuwaongoza,” alisema Kardinali Pengo.

Rais wa baraza kuu la maaskofu wakatoliki nchini (TEC) askofu wa jimbo la Mpanda, Gervas  Nyaisonga alisema askofu Lagwen ameteuliwa na Baba mtakatifu papa Francisco wakati huu ambapo wanasherehekea jubilee ya miaka 150 ya uinjilishaji.

Askofu Nyaisonga alisema askofu Lagwen baada ya kupata nafasi hiyo anapaswa kuwaangalia usoni waumini ili kuzidi kuwajenga kiroho.

Mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti alisema serikali ya mkoa huo itashirikiana na jimbo hilo katika kufanikisha ustawi wa wananchi wa eneo hilo.

Mnyeti alisema askofu Lagweni amepata daraja hilo la uaskofu ambapo ni heshima kwa wananchi wa Mbulu, Manyara na Tanzania kwa ujumla.

“Japokuwa wewe umezaliwa katika jamii ya wairaqw hata ungekuwa mmeru au msukuma lakini kwa kuwa umeteuliwa kuwa askofu wa Mbulu, umepakwa mafuta kwa uwezo wa roho mtakatifu,” alisema Mnyeti.

Akizungumza baada ya kusimikwa askofu Lagwen alisema anamuomba Mungu amsaidie kutimiza wajibu wake mpya wa kiroho katika kuwahudumia waamini wa eneo hilo.

Askofu Lagwen alisema wanashirikiana na serikali katika kufanikisha huduma mbalimbali na miradi ya elimu, afya, maji, mazingira, habari na nyingine.

Aliwashukuru wote walifanikisha tukio hilo na akawaahidi kuwa atatoa ushirikiano unaostahili kupitia nafasi yake kwa upendo na umoja watumikie.

Askofu Anthony Lagwen alizaliwa  Julai 5 mwaka 1967 kwenye Kijiji cha Tlawi, wilayani Mbulu mkoani Manyara na kuanza masomo ya elimu ya msingi na masomo ya sekondari katika seminari ndogo ya Sanu, Jimbo Katoliki la Mbulu.


from MPEKUZI

Comments