Mkuu wa chuo mbaroni akimfanyia mtihani mwanafunzi

Mkuu wa chuo cha ufundi nchini Burundi amekamatwa ndani ya chumba cha mtihani akimfanyia mtihani mtahiniwa.

Benjamin Manirambona, kutoka Chuo cha Ufundi cha Buterere kilichopo kaskazini mwa Bujumbura, ametiwa mbaroni na polisi pamoja na maofisa elimu akiwa kwenye mtihani wa mwisho.

Manirambona alikiri kutenda kosa hilo na kudai kuwa alikuwa akimfanyia mtihani huo kwa niaba ya mwanafunzi mmoja ambaye ni askari yuko kikazi nchini Somalia kwa ahadi ya malipo ambayo angelipwa baada ya askari huyo kurejea nyumbani.

Tukio hilo ambalo limeelezwa kuvunja rekodi nchini humo kwa mkuu wa chuo kufanya udanganyifu ili kumsaidia mtahiniwa apate sifa ya kuingia chuo kikuu.

Imeelezwa kuwa baada ya kupata taarifa, polisi na maofisa elimu walivamia chumba cha mtihani na kumtia mbaroni mtuhumiwa ambaye bado anashikiliwa mpaka sasa.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa na wanafunzi wengine ambao nao wanatuhumiwa kufanya udanganyifu kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa polisi kwa siri.


from MPEKUZI

Comments