BREAKING: ACT Wazalendo Walivyomjibu Katibu Mkuu wa CCM Kuhusu Uchaguzi, Ajira, Ilani ya CCM na Mengine

*Utangulizi*
Juzi tarehe 13 Agosti 2018, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Ndg. Bashiru Ally alizungumza na waandishi wa habari kuhusu kile alichokiita "shukrani kwa ushindi wa CCM" kwenye uchaguzi wa marudio Buyungu na kata 77 nchini. 

Kwenye Mkutano wake na waandishi wa habari upo upotoshaji wa wazi wazi kwenye maeneo kadhaa ambao hatukudhani kama ungetolewa na mtu wa hadhi ya katibu mkuu. Tunadhani ni muhimu sana kuweka kumbukumbu sawa kwenye maeneo yafuatayo:

A.Kuvurugwa kwa uchaguzi wa marudio
B.Utekelezaji wa Ilani ya CCM
A.Kuvurugwa kwa Uchaguzi:

Katika taarifa yake, Dk. Bashiru Ally amezungumzia aliouita ushindi wa "mia kwa mia" wa CCM kwenye uchaguzi wa marudio. Ukweli wa mambo ni kwamba CCM haijashinda kwa haki Buyungu na kwenye kata nyingi kwenye uchaguzi huu. CCM kwa kushirikiana na vyombo vya dola na Tume ya Uchaguzi wamehakikisha CCM inashinda kiharamu Buyungu na kwenye kata nyingi kama ifuatavyo;

i. Kabla ya kampeni kuanza zilifanyika njama ovu kuhakikisha wagombea wa upinzani wanahujumiwa ili CCM iweze kupita bila kupingwa. Mfano wa wazi ni wa wagombea nane wa vyama vya upinzani kwenye kata za Tunduma kutangazwa kuwa si raia ili CCM iweze kupita bila kupingwa kwenye kata hizo.

ii. Wapinzani tulibughudhiwa na mikutano yetu kuvamiwa na polisi. Mfano halisi ni wa wagombea wote wa vyama vya upinzani katika kata ya Turwa (Tarime) kuzuiwa kufanya kampeni siku mbili za mwisho ili kutoa mwanya kwa CCM kushinda.

iii. Matokeo feki kutangazwa ili kumpa ushindi mgombea wa CCM Jimbo la Buyungu tofauti na matokeo halisi vituoni.

Katika mazingira ya namna hii CCM haiwezi kutamba kuwa imeshinda kwa asilimia mia moja kama anavyosema Dk. Bashiru Ally.

B. Utekelezaji wa Ilani ya CCM:
Kwenye taarifa yake, Dk. Bashiru Ally anadai kile anachokiita ushindi wa CCM kimetokana na utekelezaji wa Ilani ya CCM ambao umeongeza imani ya wananchi. Huu ni upotoshaji.

Mwenendo wa mambo nchini unaonyesha kuwa CCM imeshindwa kabisa kutekeleza Ilani yake kwenye maeneo yake makuu. Ilani ya CCM imegawanyika kwenye maeneo makuu manne kama ifuatavyo:

i. Kupunguza umasikini
ii. Kuchochea ajira
iii. Kuimarisha ulinzi na usalama
iv. Kupunguza rushwa na ufisadi.
I. Kukithiri kwa umasikini hasa vijijini
Tofauti na tambo za Katibu Mkuu wa CCM, hali halisi ya mambo mijini na vijijini inaonyesha dhahiri kukithiri kwa umasikini.
 
Mathalani, Mwaka huu, Kiongozi wa Chama Ndugu Zitto Kabwe amefanya ziara kwenye kata zote zinazoongozwa na ACT Wazalendo ambazo nyingi zipo vijijini.

Hali ya maisha ya wananchi wetu vijijini ni mbaya sana. Kwenye kata zote ambazo zilitembelewa tumekuta tatizo kubwa ni Ardhi, Maji, Ukosefu wa Huduma za Afya, Ukosefu wa Pembejeo, Ukosefu wa soko la mazao ya wananchi, Upungufu wa vyumba vya madarasa, vyoo pamoja na walimu na kuzorota kwa hali ya usalama wa wananchi pamoja na mali zao, pamoja na uminywaji mkubwa wa demokrasia na uhuru wa watu.
 
Utafiti uliofanywa na Afrobarometer na kutangazwa na REPOA unaonyesha kuwa Watanzania 3 kati ya 10 wanalala/kushinda njaa kila siku. Kiwango hiki kimeongezeka kutoka mwaka 2014 ambapo Watanzania 2 kati ya 10 walikuwa wanakosa chakula. 

Ongezeko hili kubwa la umasikini wa Wananchi wetu tumelithibitisha kwa kuona kwenye ziara hii na linatokana kwa kiwango kikubwa na maamuzi ya kisera ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na CCM.

Maji ni tatizo kubwa sana kwa wananchi wetu. Kwa mujibu wa Utafiti wa Afrobarometer wa Taasisi ya REPOA, asilimia 42 ya Watanzania wanaona maji ni tatizo kubwa ukilinganisha na asilimia 34 ya mwaka 2014. 

Tumeshuhudia wanachi katika kata nyingi tulizotembelea wakikabiliwa na tatizo la uhaba mkubwa wa maji. Tatizo hili linasabibisha kukwamisha shughuli za maendeleo za wananchi katika maeneo yao. 

Aidha wananchi wamekuwa hawapati huduma ya uhakika ya maji safi na salama hivyo kupelelekea kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko yanayosababishwa na unywaji wa maji yasiyo safi na salama.

Wahanga wakubwa ni kina mama ambao hulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya maji. Baadhi ya maeneo wananchi wanalazimika kutumia maji katika visima visivyo salama ambavyo hutumika kunyweshea wanyama mfano kata ya Tomondo wakitumia visima ambavyo wanyama pia wanakunywa maji humo humo.
 
Bei ya maji pia katika maeneo mengi ya vijiji imekuwa kubwa kulinganisha na watumiaji wa maji mijini. Hivyo kwa baadhi ya maeneo kipato chote cha mwananchi hutumia katika kupata huduma ya maji ( Gehandu Pipa la Lita 200 Tsh 7,000). 

Hali hii inafukarisha zaidi wananchi kwani licha ya kuwa na kipato duni wanalipa Maji zaidi ya mara 10 ya watu wenye kipato kikubwa mijini. Hili linakuza sana pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho (Inequality) kati ya wakazi wa mijini na wakazi wa vijijini.

II.Kuendelea kushamiri kwa Janga la Ajira:
Ni upotoshaji pale Katibu Mkuu wa CCM anaposema CCM imeboresha ajira. Ajira zipi?
Serikali ya awamu ya tano inafahamika kuwa kinara wa kupunguza ajira, kuweka mazingira duni ya vijana kujiajiri na kuwa na mazinugira duni kwa wafanyakazi walioajiriwa.
 
Sasa ni mwaka wa tatu serikali haijaajiri kwa kiwango kilichozoeleka huko nyuma kwa kisingizio cha uhakiki na baadaye kutumia fedha kwenye miradi ya maendeleo. Ni ajira gani anazozisema Dk. Bashiru?

Inafahamika kwamba vijana wanaoingia kwenye soko la ajira kwa mwaka ni 800,000 na wanaopata ajira ni 70,000 tuu. Hii ni dalili ya wazi ya CCM kushindwa kukabiliana na changamoto ya ajira.

Hata ahadi ya Mil. 50 kwa kijiji ambayo ingesaidia kuboresha ajira vijijini nayo imeota mbawa.

III.Kuendelea kwa vitendo vya rushwa na ufisadi:
Licha ya tambo za Serikali ya CCM kuwa sasa inapambana vilivyo na rushwa na ufisadi, kuna dalili za wazi za kuendelea kwa ufisadi mkubwa nchini. Mfano wa wazi ni ule ulioainishwa kwenye Ripoti ya CAG ya Mwaka 2016/2017 ambapo ilioneshwa wazi kuwa jumla ya Tsh. 1.5 Trilioni zimetumika bila kuidhinishwa na Bunge. Kama kweli Serikali ya CCM inachukia rushwa na ufisadi ituoneshe wapi zilipo 1.5 Trilioni zilizosemwa na CAG

IV.Kudorora kwa Usalama wa Raia:
Chama chetu kinaheshimu kwa dhati mchango wa vyombo vya ulinzi na usalama ndani na nje ya nchi. Lakini, hiyo haiondoshi ukweli kwamba hali ya usalama wa raia hivi sasa ni mbaya sana kuliko kipindi kingine chochote cha uhuru wetu.
 
Tunaishi zama ambazo wanasiasa (Kama vile Simon Kanguye, Ben Saanane, Tundu Lisu) wanapotezwa/kushambuliwa kwa risasi mchana kweupe halafu vyombo vyetu vya ulinzi na usalama havina majibu ya kueleweka.

Tupo kwenye zama ambazo waandishi wa habari wanashambuliwa na askari na wakubwa wa jeshi la polisi wanawatetea askari hao.

Hizi ni zama ambazo mamia ya wananchi wamepotezwa kwenye operesheni ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji na serikali haina majibu. Huu ndio usalama anaouzungumza Dk. Bashiru?

*Hitimisho*

(i). CCM haijatekeleza hata robo ya ahadi zake;
Ilani ya CCM ina aya 189 zilizo sheheni ahadi mbalimbali. Katibu Mkuu wa CCM anaposema nusu ya ahadi zimetekelezwa atuonyeshe kwa uthibitisho kuwa nusu ya aya 189 zimetekelezwa mpaka sasa. Sisi tunaamini kuwa Katibu Mkuu wa CCM amejisemesha tu na neno nusu limemtoka tu kwani kwa mujibu wa utafiti wetu na ufuatiliaji CCM haijatekeleza hata robo ya ahadi zake mpaka sasa mwaka wa tatu unakatika tangu waingie madarakani

(ii). CCM haijashinda, imejitangazia ushindi kimabavu kwa kushirikiana na vyombo vya dola na Tume ya Uchaguzi

(iii). CCM ijue kuwa inapofunga mlango wa wananchi kuchagua viongozi kwa njia ya kidemokrasia, inafungua milango mingine ambayo inaweza kuitumbukiza nchi yetu kwenye machafuko. Hili si jambo lenye afya kwa taifa.

*Mapendekezo*

(i). Uitishwe Mkutano wa Kitaifa wa maridhiano ya kisiasa ambapo changamoto zote za uendeshaji wa siasa nchini zijadiliwe na kukubaliana kanuni za demokrasia ya vyama vingi.
(ii). Tufanye mabadiliko makubwa kwenye mfumo wa siasa na vyombo vya dola, ikiwemo
- Kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi
- Mabadiliko makubwa ya Jeshi la Polisi ili kulifanya kuwa linatoa huduma ya kulinda raia badala ya kutesa raia (Police Service badala ya Police Force), na
- Mabadiliko makubwa ya Kitengo cha Usalama wa Taifa ili kihusike na kulinda usalama wa Dola letu badala ya kuwa chombo cha chama kimoja cha siasa.
(iii). Iundwe Tume Huru ya Uchunguzi ili kuchunguza matukio yote ya mauaji ya raia kuanzia Kibiti mpaka mauaji ya siku za karibuni ya raia wa kawaida, viongozi wa kisiasa na hata majaribio ya kuua baadhi ya wabunge ambao wengine sasa wapo hospitali wakiendelea na matibabu.
 
Mapendekezo Mapendekezo Tunasisitiza kuwa mapendekezo haya yafanyiwe kazi kwa salama ya nchi yetu. Vinginevyo nchi inakwenda kupata tabu sana kuelekea 2020.

Dorothy Semu,
Kaimu Katibu Mkuu,ACT Wazalendo
15 Agosti 2018


from MPEKUZI

Comments