Waziri mwakyembe atofautiana na TFF ongezeko la wachezaji 10 wa kigeni badala ya 7.

Na Magdalena Kashindye
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amesema hakubaliani na uamuzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wa kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni kufikia 10 kwenye vilabu vya soka nchini na  ameliagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuwahoji TFF kuhusu msingi wa uamuzi huo na kutaka utaratibu wa awali uendelee.

Akihojiwa na wanahabari wilayani Kyela ambako ana ziara ya kikazi katika jimbo lake la uchaguzi, Dk. Mwakyembe amesema alitegemea TFF kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni kutoka 7 hadi watano au chini yake na  si vinginevyo.

"Hili ni suala la ki-sera linalodai ushirikishwaji mpana wa wadau ikiwemo Serikali na vyombo vyake, si la TFF peke yake kuamua", amesema mwakyembe

Utaratibu uliokuwepo awali ni wa klabu kusajili wachezaji wa kigeni wasiozidi saba na kati ya hao watano tu kuweza kuchezeshwa katika mchezo moja.

Lakini kwa mabadiliko yaliyotangazwa wiki iliyopita na TFF, timu inaweza kuwasajili na kuwatumia wachezaji wote 10 kutoka nje katika mchezo moja, hatua ambayo Dk. Mwakyembe amesema itaua vipaji vya ndani kwa maslahi finyu ya vilabu vikubwa vyenye ukwasi.

"Binafsi sioni hoja yoyote yenye mashiko kuhalalisha ongezeko hilo la wachezaji wa kigeni nchini. Ninachokiona hapa ni kuwapunguzia fursa vijana wa Kitanzania uzoefu kuchezea klabu kubwa nchini na hivyo kuinyima Timu ya Taifa vipaji vipya vya Kitanzania vinavyotokana na michuano mikali ya Ligi Kuu", amesisitiza. amesema mwakyembe.


from MPEKUZI

Comments