Waziri Kigwangalla Awataka Wavamizi Maeneo Yaliyohifadhiwa Kuondoka

Na Pamela Mollel,Arusha
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla amewataka wananchi waliovamia maeneo ya hifadhi nchini, kujiandaa kuondoka ndani ya miezi mitatu kabla ya operesheni kuanza.

Akizungumza na waandishi wa habari,Julai 19  katika eneo la  hifadhi ya Jamii ya wanyamapori(WMA) ya makao, wilayani Meatu, Dk Kigwangalla alisema wavamizi wa maeneo ya hifadhi wengi wamekuwa wakijihusisha na matukio ya ujangili.

“Utakula kijiji kina ardhi kubwa, lakini wengine wanajenga hadi katika ndani ya eneo la mita 500 kutoka mpaka wa hifadhi na hao mara nyingi ndio wanaingiza mifugo hifadhini usiku na kufanya ujangili”alisema

Alisema maeneo mengi ya hifadhi na mapori ya akiba nchini yamevamia na wananchi jambo ambalo serikali haiwezi kukubali yaharibiwe ama kutumika kwa ujangili.

Waziri huyo, pia alitembelea kambi ya kitalii ya TGTS na hoteli ya  Mwiba   na kushuhudia vikosi vya kupambana na ujangili katika maeneo hayo ambavyo vipo yapo chini ya taasisi  Friedkin Conservation Fund na kueleza kuridhishwa na uwekezaji wa taasisi hiyo.

Mkurugenzi wa Mwiba Holding, Abdukaril Mohamed, alisema katika eneo la Mwiba wamewekeza sh 2.2 bilion na hivi sasa wanaendelea na shughuli za uhifadhi na utalii.

“Mheshimiwa Waziri katika eneo hili, kampuni yetu inafanya utalii wa picha na kuna hoteli,tunafanyakazi kwa amani na utulivu na vijijini vinavyotuzunguka”alisema

Mwenyekiti wa kijiji cha makao, Anthony Philip, alimweleza Waziri Dk Kigwangalla kuwa, katika eneo hilo kuna mahusiano mazuri baina ya vijiji na wawekezaji na vijiji vinapata mgao wa fedha.

Alisema kijiji cha makao kimekuwa kikipata zaidi ya sh 147 milioni kwa mwaka kutoka kwa mwekezaji na vijiji vingine sita vimekuwa vikipata zaidi ya milioni 80,000 kila mwaka”alisema.

Akiwa katika pori la akiba la Maswa,Meneja wa pori hilo, Lusato Masinde alisema pia wanauhusiano mzuri na wawekezaji ambao licha ya kulipia ada za vitalu pia wamekuwa wakitoa msaada wa huduma mbali mbali ikiwepo maji.

Hata hivyo, alisema katika pori hilo changamoto kubwa ni uvamizi wa mifugo, uchache wa watumishi na upungufu wa vitendea kazi.

Mwisho.


from MPEKUZI

Comments