Wazazi 5 wenye watoto wahalifu watiwa mbaroni

Kutokana  na kukithiri kwa vitendo vya uhalifu katika mtaa wa Kisasa jijini Dodoma, Jeshi la Polisi limelazimika kuwakamata wazazi watano wa vijana wanaojihusisha na matukio hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma Gilles Muroto, alisema amelazimika kuwakamata wazazi na walezi wa vijana hao baada ya kuwatoroka polisi.

“Jeshi la Polisi litawashughulikia wazazi wanaowahifadhi wahalifu katika familia zao, tumebaini kuwa wapo baadhi ya wazazi wamewatorosha wahalifu na mimi ninaagiza wawasalimishe haraka iwezekanavyo,” alisema.

Alisema wazazi wanao wajibu wa kuwalea watoto wao vizuri na kutoa taarifa polisi za uhalifu kwa kuwa wanajua wanapora mali za watu na kuvunja nyumba.

“Tunajua kuna baadhi ya wazazi wanawalinda na kuwahifadhi wahalifu hao lazima tukomeshe vitendo vya kihalifu Dodoma,” alisema. 

Alibainisha kuwa Dodoma ni salama kwa watu wema na si salama kwa wahalifu wa aina yoyote na kuonya kuwa wasiokuwa tayari kubadilika watakamatwa na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Muroto alisema jeshi hilo litaendelea kufanya operesheni kwa ajili ya kuabaini makundi ya wahalifu ambao ni vijana wanaoishi katika maeneo mbalimbali wanaojihusisha na uporaji wa mali za watu.

Alisema katika operesheni hiyo itawahusisha kuwakamata watu wanaowafahamu wazazi na walezi wanaowalinda watoto wahalifu.

Hivi karibuni wakazi wa mtaa huo na maeneo mengine ya jirani wamekuwa wakilalamika nyumba zao kuvunjwa na kuibiwa vitu mbalimbali ikiwamo runinga pamoja na kutishiwa uhai.

Mmoja wa wakazi hao, Debora Fredy, alisema kila wakati kumekuwapo na matukio ya uhalifu kwenye mtaa huo na kuhitajika kuwapo msako wa usiku kwenye mitaa ili kuifanya Dodoma kuwa shwari.

Alisema wengi wa wakazi wanalalamika kuporwa mali zao na wengine kuvunjiwa nyumba na kuibiwa vifaa mbalimbali hususan runinga za kisasa (flat screen).


from MPEKUZI

Comments