Serikali Yaahidi Kuweka Mazingira Bora Kwa Sekta Binafsi Nchini

Serikali imeahidi kuweka mazingira wezeshi yatakayorahisisha sekta binafsi kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya maji.

Ahadi hiyo imetolewa jana Ijumaa Julai 20, 2018 na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji,  Jumaa Aweso wakati wa kufunga kongamano la wadau wa sekta ya maji.

Amesema kupitia kongamano hilo imeonekana kuna haja ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha changamoto ya maji inapatiwa ufumbuzi.

“Tunatambua changamoto zinazoikabili sekta binafsi, tutazifanyia kazi na kuangalia namna bora ya kukabiliana nazo lengo ni kuhakikisha maji yanapatikana ya kutosha,” amesema.

Kongamano hilo la siku mbili lililenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuendeleza sekta ya maji nchini lililobebwa na kauli mbiu 'maji ni uchumi'.

Naye Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, mhandisi Stella Manyanya amewataka wakandarasi kuwa na taarifa za kutosha kuhusu vifaa vinavyopatikana ndani ya nchi.

Amesema hilo litapunguza kasi ya kuagiza vifaa kutoka nje ya nchi na kutoa fursa kwa wazalishaji wa ndani kuuza vifaa vyao.

"Tunapenda kuona viwanda vinavyozaliwa Tanzania vinakuwa, wale watafiti wasikimbilie kusema vifaa vya ndani havina ubora ni jukumu lao kufanya utafiti kujua ubora na nini kifanyike viwe bora,” amesema.

“Kuanzia sasa zikitolewa zabuni kubwa za miradi ya maji, wizara ya viwanda tutapita kuangalia ni vifaa gani vimetumika na vimetolewa wapi.”

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo amesema Serikali itafanya kila linalowezekana kuiwezesha sekta binafsi kufanya kazi ila sio kuilea.

Akizungumza kwa niaba ya sekta binafsi, Mkurugenzi wa Huduma kwa wanachama Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Luis Akaro ameitaka Serikali kuweka mazingira wezeshi katika ufanyaji biashara unaohusisha sekta ya maji.

Amesema kufanikiwa kwa kongamano hilo ni dhahiri kuwa Serikali imedhamiria kukabiliana na changamoto ya maji.


from MPEKUZI

Comments