Serikali Kutovivumilia Vyuo Vitakavyotoa Mafunzo Kinyume Na Utaratibu

Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), kutovibembeleza vyuo visivyo na sifa, badala yake ivichukulie hatua kali ikiwamo kuvifungia.

Pia ameitaka kuhakiki kwa makini vyuo vikuu vyote na kuvichukulia hatua vitakavyobainika kukiuka utaratibu wa utoaji wa elimu.
 
Hata hivyo, wadau wa elimu waliozungumzia hatua hiyo wamesema imechelewa kuchukuliwa kwani tayari kuna wahitimu kutoka vyuo hivyo wasio na sifa.
 
Profesa Ndalichako alitoa maagizo hayo jana katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini hapo, alipozindua maonyesho ya 13 ya elimu ya juu, sayansi na teknolojia yenye kaulimbiu “Elimu ya Juu Bora kwa Mapinduzi ya Viwanda.”
 
Alisema, “Katika awamu hii watu wanaofanya kazi kwa mazoea hawana nafasi, lazima muwe wabunifu na mpitie upya zana mnazotumia kuhakiki ubora wa vyuo, inawezekana zina matobo.”
 
Alisema Serikali itaendelea kuimarisha mfumo wa ithibati na udhibiti wa ubora wa elimu na mafunzo ili kuhakikisha asilimia kubwa ya wahitimu wa shahada wanachangia ukuaji wa uchumi kulingana na elimu waliyopata.  
 
 “Katika ubora wa elimu hatutakuwa na mzaha, naomba hilo lieleweke vizuri kwa wadau wote, ili kuimarisha elimu tunapaswa kufanya kazi kwa pamoja,” alisema.
 
Alisema Serikali na wadau wengine wa elimu ya juu kila mmoja atimize wajibu wake. “Tuwe na uzalendo, elimu isiwe ni biashara, bali fursa ya kuendelea.”
 
Profesa Ndalichako alisema Chuo Kikuu cha Kenyatta kiliamua kufunga tawi la Arusha baada ya matokeo ya uhakiki kuonyesha udhaifu, huku tawi la Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira Mbeya likifungwa Julai 5.
 
“Natoa wito kwa taasisi zote za elimu ya juu ambazo matokeo ya uhakiki yalibainisha zina upungufu zifanyie marekebisho kasoro hizo haraka iwezekanavyo kama walivyoelekezwa na mamlaka za ithibati. Vinginevyo hatua stahiki zitachukuliwa, ikiwa ni pamoja na kufuta usajili wa vyuo hivyo,” alisema.
 
Mwakilishi wa kamati ya vyuo vikuu, Profesa Yonica Ngaga alisema hatua ya kuvidhibiti vyuo visivyo na sifa imechelewa kuchukuliwa kwa sababu tayari vimetoa wahitimu walio kwenye kampuni na taasisi kadhaa.
 
“Hatua hii ilipaswa kuchukuliwa mapema. Hata hivyo, si vibaya kwa sababu tayari TCU inachukua hatua, itasaidia kudhibiti uzalishaji wa wasomi wasio na sifa,” alisema.
 
Alisema baadhi ya vyuo vilianzishwa kwa sababu ya uwapo wa Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa kuwa wengi watakuwa na uwezo wa kulipa ada.
 
“Vipo vinavyoshindana kwa wingi wa wanafunzi na hawajishughulishi kuangilia wahitimu wao ni mahiri kiasi gani kwenye masoko ya ajira, matokeo yake wahitimu wao wengine ni mabomu wakipewa kazi wanaharibu kwa kuwa hawana uwezo,” alisema.
 
Katibu mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa alisema maonyesho hayo yameshirikisha taasisi 68 za elimu ya juu zikiwamo nne kutoka nje ya nchi.


from MPEKUZI

Comments