Peter Msigwa: Upinzani ukifa watumishi watapata tabu sana

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema ikifika mahali vyama vya upinzani nchini vikafa, ni dhahiri watumishi wa umma wakiwamo wa Manispaa ya Iringa watapata tabu sana.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini Mch. Peter Msigwa, jana kwa waandishi wa habari wakati akizungumzia madai kuwa kuna hujuma zimefanywa na baadhi ya wana CCM Manispaa ya Iringa katika uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata tano.

Alidai kuwa baadhi ya watumishi wa serikali kwa makusudi wanashinikizwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhujumu Chadema ili ishindwe katika uchaguzi mdogo, hivyo wasidhani kuwa kukihujumu chama hicho kikuu cha upinzani kutawafanya wao wabaki salama, ukweli hawatobaki salama kama wanavyofikiri.

Katika uchaguzi huo Manispaa ya Iringa kata mbili za Kwakilosa na Gangilonga wagombea wa CCM wamepita bila kupigwa.

Msigwa alisema kutokuwapo kwa siasa za upinzani nchini, hakuna taasisi itakayobaki salama kwani hata wana CCM wanaoshangilia wataathirika kwa kiasi kikubwa.

“Nataka niwaambie watumishi wa serikali, kufa kwa Chadema, kutokuwapo kwa siasa za upinzani, kutokuwapo kwa Chadema watapata tabu sana katika kipindi cha miaka mitano ambayo Chadema imeongoza halmashauri chini ya Meya Alex Kimbe, wataalamu wamefanya utaalamu wao kwa weledi kwa sababu wamekuwa huru,” alisema na kuongeza:

“Tumedhibiti wizi, lakini sasa hivi wanadhani kutoa Chadema au upinzani wao watakuwa salama ila watambue watapata tabu sana.”

“Mimi nisema wazi kuna wakurugenzi na watendaji wamejigeuza kuwa makada wa CCM bila hata ya kificho kama huyu mkurugenzi wa Iringa anashindwa kufuata taratibu za uchaguzi na kuna fomu zetu, amezikataa kabisa na kuziwekea pingamizi wakati hiyo siyo kazi yake.

“Maana pingamizi huwekwa na mgombea na sio msimamizi wa uchaguzi, mimi niwambie wasijione wako salama wanapotuhujumu, bali wanajipalia moto,” aliongeza.



from MPEKUZI

Comments