Mgunduzi wa Madini ya Tanzanite Aliyepewa Mil. 100/- na Rais Magufuli apelekwa India

Mgunduzi  wa madini ya Tanzanite, Jumanne Ngoma, ambaye anasumbuliwa na maradhi ya kupooza amepelekwa India kwa ajili ya matibabu.

Mzee Ngoma alisafirishwa juzi na tayari jana alianza kupata matibabu katika Hospitali ya Apollo jijini New Delhi.

Kwa mujibu wa mtoto wa mzee huyo, Asha Ngoma, mgunduzi huyo ameamua kutafuta matibabu zaidi baada ya kutibiwa hapa nchini.

“Alipata matibabu nchini, lakini ameamua kutafuta matibabu zaidi nje ya nchi ili aone kama atapona haraka zaidi,” alisema mtoto huyo na kuongeza:

“Mzee amekuwa akipatiwa matibabu tangu wakati ule Rais Magufuli alipompatia Sh. milioni 100 Aprili mwaka huu kwa ajili ya matibabu zaidi wakati wa uzinduzi wa ukuta wa Mirerani.”

Alimshukuru Rais Magufuli kwani walipewa fedha hizo ndani ya muda mfupi zilimsaidia sana.

Aprili 6 mwaka huu, Rais Magufuli akiwa mji mdogo wa Mirerani Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wakati akizindua ukuta uliozunguka machimbo ya madini ya Tanzanite, alitangaza kumtambua Mzee Ngoma na kumwahidi kumpatia fedha hizo ili zimsaidie katika matibabu.

Akizungumza na wananchi siku hiyo, Rais Magufuli alisema atamwandikia barua maalum ya kumtambua Mzee Ngoma.

Rais Magufuli alisema alipata ujumbe mfupi na baadaye kupata taarifa kutoka kwa mtoto wake, Hassan na alipofuatilia alibaini ni za kweli.

“Nimeambiwa tangu mwaka 1967 madini haya yagunduliwe na mzee huyu, lakini pamoja na kutambuliwa na Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere kwenye barua niliyoiona iliyosainiwa tangu tarehe 3/8/1980 na nakala yake ya kuvumbua madini ya aina ya pekee na kuyapeleka kwa mtaalam wa madini na miamba mwaka 1967, barua hiyo nayo ninayo hapa,” alisema.



from MPEKUZI

Comments