Mbunge wa Zamani CUF Ajiunga CCM

Mbunge wa zamani wa viti maalumu (CUF), Amina Mwidau amejivua uanachama wa chama hicho na kutangaza kujiunga na CCM.

Amina katika taarifa aliyoisambaza kwenye vyombo vya habari jana, alisema sababu ya kuhama CUF ni kutaka kujipanga kivingine katika safari ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Alisema baada ya miaka miwili na nusu ya kutafakari mwenendo wa kisiasa ndani ya CUF na vyama vingine vya upinzani, pamoja na utendaji wa Serikali ya awamu ya tano ameamua kujivua uanachama wa chama hicho.

“Nimeridhika sasa ni wakati muafaka wa kujipanga kivingine katika safari ya kushiriki kuleta maendeleo na ustawi wa wananchi wote,” alisema.

Amina aliyekuwa mbunge mwaka 2010 hadi 2015 na aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema ameamua kujiunga na CCM kwa sababu ana ndoto ya kuendelea kushirikiana na wananchi katika kuleta ustawi na maendeleo, hivyo hayupo tayari kuishia njiani.


from MPEKUZI

Comments