Magereza Na JKT Kushirikiana Katika Miradi Ya Uzalishaji Mali

Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa wameahidi kushirikiana katika miradi mbalimbali ya uzalishaji mali kupitia mashirika yake ya Magereza Corporation Sole na SUMA-JKT.

Hayo yamejiri wakati wa ziara ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Phaustine Kasike  alipomtembelea Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Matin Busungu ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake  za kujitambulisha kwa viongozi mbalimbali wa kitaifa tangu ateulie kuwa mkuu wa Jeshi hilo Julai13, 2018.

Katika mazungumzo yao, wakuu hao wa taasisi hizo muhimu nchini wameonesha utayari wa ushirikiano katika miradi ya ujenzi pale taasisi moja inapokuwa na miradi mikubwa inayoweza kuhitaji utaalam au nguvu ya kuweza kushirikiana.

Aidha, Meja Jenerali Busungu amesema kuwa JKT  lipo tayari kulikopesha matrekta Jeshi la Magereza wakati litakapokuwa limekamilisha  mpango wake kilimo cha kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa kama ilivyoelekezwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli.

“Namshukuru sana  Meja Jenerali Busungu kwa kuonesha utayari wa kushirikiana na Jeshi la Magereza, kilichobaki ni kujipanga na kuanza utekelezaji mara moja”. Amesema Jenerali Kasike.


from MPEKUZI

Comments