Bucha bubu za mbuzi Zaitesa Halmashauri ya Mji wa Kahama

Na Magdalena Kashindye
Kuwepo kwa bucha bubu za mbuzi katika halmashauri ya mji wa Kahama mkoani Shinyanga imekuwa  ikiisababishia hasara katika halmashauri hiyo kutokana na baadhi ya watu kuchinja  mbuzi mtaani na nyumbani kwa lengo la kukwepa kulipa kodi.

Hayo yamebainishwa na Afisa Mifugo wa halmashauri ya mji wa Kahama Costantine Lugendo wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisi kwake.

Lugendo amesema kuwa takwimu zinaonesha kuwa uchinjwaji wa mbuzi  umekuwa ukidorora kutoka mbuzi 60 na kufikia mbuzi 20 pekee kwa siku katika machinjio rasmi lakini upatikanaji wa nyama hiyo umekuwa ukiongezeka mtaani.

 Afisa mifugo huyo amekili  kuwa kuna tabia kwa baadhi ya watu wamekuwa wakichinja mbuzi  mtaani au nyumbani na kupeleka kwenye migahawa kuuza nyama  kwa lengo la kukwepa kulipa kodi.

Bwana Lugendo amesema kuwa idara Ya mifugo inafanya mkakati wa kuweka askari watakaofanya doria ya kuwakamata watu wanaochinja mifugo  mtaani kwa ajili ya nyama ya kuuza  ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Hata hivyo Lugendo amesema kuwa uchinjaji  na  uuzaji wa nyama  ovyo bila kukaguliwa na maafisa mifugo  ni hatari kwa afya ya Mlaji kwani haijulikani imechinjwa katika mazingira gani huku pia halmashauri kushindwa kupata mapato ya mifugo.

Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania imefanya utaratibu maalum wa uchinjaji wa mifugo katika machinjio  maalum yaliyorasimishwa na serikali  ili kulinda afya ya mlaji.



from MPEKUZI

Comments