Wakuu wa Miko na Wilaya Wanaofukuza Watumishi wa Umma Kuchukuliwa Hatua

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora, Kapteni (Mstaafu), George Mkuchika ameomba kama kuna mahali mtumishi amefukuzwa kazi na Mkuu wa Mkoa wa Mkuu wa Wilaya wakati si waajiri wake apelekewe suala hilo na yeye atalishughulikia.

Mkuchika ametoa ombi hilo leo, Juni 18, 2018 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini aliyeuliza “Katika awamu hii umezuka mtindo kwa baadhi ya wakuu wa mikoa na Wilaya kuwavua vyeo baadhi ya walimu kutokana na sababu ya shule zao kutofanya vizuri, kuwavua vyeo madaktari na hata wengine kuwaondoa kazini na sasa mtindo huu unavyoendelea tafsiri ya jamii ni hatua ambazo ni mahususi zilizoagizwa na serikali , Je serikali ipo tayari kupitia maamuzi yote haya na kuwarejea hawa walimu au madaktari haki yao kama ilidhibitika walionewa?

Akijibu swali hilo Mkuchika amesema kuwa “Nchi hii inaendeshwa kwa sheria, taratibu na kanuni lakini ni kwamba yule aliyekuajiri wewe ndiye mwenye madaraka ya kukufukuza kwahiyo utaona kwamba mara nyingi wakigundua kama kuna makosa wana msimamisha wakati wanasubiri yule mwenye madaraka ya ajira achukue hatua za mwisho.”

Pia aliomba kuwa “Ninaliomba Bunge hili kama kuna mahali mtumishi amefukuzwa na Mkuu wa mkoa au Mkuu wa wilaya wakati yeye sie aliyemuajiri niletewe suala hilo nitalishughulikia mara moja kwasababu kwa taratibu zetu za kiutumishi yule aliyekuajiri ndiye anaekuadhibu.”


from MPEKUZI

Comments