Waislamu Waaswa Kutunza Amani Na Kudumisha Mshikamano

Na Baltazar Mashaka, Mwanza
WAISLAMU wameaswa kutunza amani na utulivu uliopo nchini na wawe mstari wa mbele kuhubiri amani, utulivu na kudumisha umoja lakini itashangaza kuona baadhi yao wakiwa chanzo cha vurugu na mifarakano.

Pia wameshauriwa kuwasomesha watoto bila kuwabagua watoto  wa kike ili nao waajiriwe na kushika nyadhifa za juu serikalini na kwenye taasisi mbalimbali za umma na binafsi kwa sababu hakuna mahali popote Waislamu wamezuiwa kuwapa elimu ya mazingira watoto wao.

Kauli hiyo ilitolewa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kuendeleza Quraan na Suna Tanzania  (JUQUSUTA) ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza Sheikh Hassan Kabeke kwenye swala Idd el Fitri ilyofanyika jana Uwanja wa Shule ya Msingi Mbugani, Mwanza.

Alisema Waislamu wana wajibu wa kutunza amani na utulivu, iwe kwenye nyumba za ibada ama nyumbani na kuonya kuwa Muislamu wa kweli hapaswi kuwakosesha watu wengine amani kwa ulimi wake ikizingatiwa Uislamu ni utulivu na amani na hivyo wanapaswa kulinda na kudumisha mambo hayo mawili.

“Uislamu ni dini inayojipambanua kwa amani na utulivu na itashangaza kwa watakaokuwa chanzo cha vurugu na kuanzisha mifarakano, jambo linalokwenda kinyume na Uislamu. Mtu wa namna hiyo uislamu wake utakuwa wa shaka na wenye walakini maana leo baadhi ya nchi watu hawawezi kuabudu misikiti wala uwanjani sababu ya amani kukosekana,”alisema Sheikh Kabeke.

Alisema mbali na kutunza amani wazazi wanawajibika kuwasomesha watoto kwa kuwapa elimu ya mazingira na hata watoto wa kike wasome ili wapate nyadhifa za juu na kuwataka wazazi kuacha kuwabagua watoto kwa kuwaona baadhi ni bora kuliko wengine.

Mwenyekiti huyo wa JUQUSUTA alisema baada ya mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani kumalizika ni vyema Waislamu waendelee kumcha Mungu na kuyaishi waliyoyafanya wakati wa funga kwa kuwa Mungu anawataka kumcha yeye na itakuwa ajabu wakirejea kufanya maasi.

“Tufanye matendo yetu kwa mujibu wa swala na tufanye kazi halali ya kutupatia kipato kwa bidii tukitumia neema maana iko dhambi haisamehewi kwa funga wala sadaka badala yake kwa thawabu kwa mtu anayetafuta riziki yake kwa halali,”alisema Mwenyekiti mwenza huyo wa kamati ya amani ya viongozi wa dini.

Sheikh Kabeke aliwashauri wanaume wa dhehebu hilo kuacha kuwadhalilisha wanawake kwa kuwa kufanya hivyo wanaudhalilisha Uislamu hali kadhalika wanawake nao wawaheshimu waume zao na kipindi hiki nyumba za waislamu zisiingie kwenye migogoro, watunze familia zao kwa kuzingatia maadili ili kuwe na utulivu maana neema ya uislamu kufunga ni kupata afya.

Aidha, Aliwataka  waumini wa dini hiyo ya kiislamu kumunga mkono Mufti Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakary bin Zuberi kwa kazi ya kuwaletea maendeleo na kujenga uchumi wa waislamu na kuiimarisha BAKWATA.

Pia aliwataka waislamu kuacha kuzozana kwa kufanya hivyo watadhoofika na hata mafanikio watakayoyapata nje ya umoja hayatakuwa mafanikio na hivyo wasimame pamoja ili kuleta maendeleo ya dini yao na taifa na mtu atakayetaka kuwavuruga wasimpe nafasi.

Ibada hiyo ya Idd El Fitri ilifanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Mbugani katika Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza na kuendeshwa na Sheikh wa wilaya hiyo Othman Ramadhan.


from MPEKUZI

Comments