Sugu aelezea kuteswa na watu wa Mbeya

Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi (Sugu) ambaye pia ni msanii nguli na mkongwe kwenye game ya hip hop ya bongo, ametimiza ahadi yake ya kutoa nyimbo aliyoipa jina la namba yake ya jela, 219 ambayo ndani yake ameelezea matukio mbalimbali anayokutana nayo ndani ya siasa.

Sugu ameachia kibao hicho jana Juni 15, 2018 baada ya kupita takribani siku 13 tokea alipotoa kauli yake ambayo ilikuwa kama ahadi kwa mashabiki wake wa muziki pamoja na wananchi wa Mbeya kuwa atatoa wimbo ambao utakuwa unazungumzia hali ya nchi na masuala mbalimbali anayokutana nayo katika siasa.

"Mfungwa wa kisiasa 219 Mbeya ndiyo inanitesa (wanaitaka Mbeya), najua Mbeya ndiyo inanitesa lakini bado napenda Mbeya inavyonitesa. 

"Muziki sikuchagua bali ulinichagua nikafanya kweli na dunia ikanijua, siasa sikuichagua, amini usiamini siasa ndiyo ilinichagua na iliponichagua Mbeya wakanichagua, kwa mara nyingine tena dunia ikanitambua na wale wasioamini wakaamini imeshakuwa", haya ni miongoni mwa mashairi yanayosikika katika wimbo huo wa Sugu.

Sugu alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miezi mitano mnamo Februari 26, 2018 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kwa kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Disemba 30, 2017 eneo la Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya na ilipofika Mei 10, 2018 Sugu aliachiwa kwa msamaha wa Rais na kutoka katika Gereza Kuu la Ruanda mkoani Mbeya alikokuwa akishikiliwa.


from MPEKUZI

Comments