Polisi yatoa onyo magari ya Serikali yanayovunja sheria

Jeshi la Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam limesema linaanzisha operesheni maalum kuanzia leo Juni 14,2018 ya kukamata magari yote yatakayopita katika barabara za mwendokasi yakiwemo magari ya serikali kwa madai wao ndio wamekuwa watu wakubwa wa kuvunja sheria.

Hayo yameelezwa na Kamanda Lazaro Mambosasa leo Jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari na kusema kumekuwa na tabia ya vyombo vya moto kutumia barabara zisizo kuwa rasmi kwa wao kutumia bila ya kuwa na dharula yoyote huku akitolea mfano wa gari la wagonjwa lililosababisha ajali hivi karibuni na kuua wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kipindi linawakimbiza kuwapeleka hospitalini eneo la River Side, Ubungo Jijini Dar es Salaam.

"Kumekuwa na tabia sasa ambayo inataka kuota mizizi watu wanahama kwenye barabara husika wanaingia kwenye barabara ya mwendokasi. Barabara hiyo imetengwa kwaajili ya mabasi ya kwenda haraka lakini sasa hivi vyombo vya ulinzi na usalama, madereva wote wanataka kupita katika njia hiyo", amesema Kamanda Mambosasa.

Pamoja na hayo, Kamanda Mambosasa ameendelea kwa kusema "nitoe wito na onyo ni vema barabara zikatumika kwa mujibu wa sheria, maeneo ambayo yana makatazo tusilazimishe kufanya hivyo, nitaendesha opereshe kali na kuhakikisha hili linafanyika na mtu yoyote akikamatwa asipige makelele ninaeleza kila mtu aelewe, magari ya serikali ndio yanaongoza katika hili na hakuna sababu yoyote ya msingi kufanya hivyo".

Kwa upande mwingine, Kamanda wa Kanda maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amewataka wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao wakati wa kuvuka barabara kipindi hiki cha kuelekea Sikukuu ili ajali zisizokuwa za lazima zisitokee.


from MPEKUZI

Comments