Nape aisifu Serikali asema bajeti imezingatia vigezo

 Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye, amesema kuwa mapendekezo ya bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019 imekuwa nzuri na ipo kimkakati zaidi ukilinganisha na bajeti za miaka miwili iliyopita.

Nape amesema hayo wakati wa kutoa maoni kuhusu mapendekezo ya bajeti kuu ya serikali na kusemna kuwa serikali kwasasa imejifunza kupitia bajeti mbili zilizopita kwa kufanya marekebisho mbalimbali hasa katika mifumo ya kodi.

“Mapendekezo ya Bajeti ya Serikali 2018/2019 ina mambo mengi mazuri, zipo changamoto kadhaa lakini mambo mengi mazuri, inavyoonekana Serikali imejifunza kutoka bajeti ya kwanza na ya pili, kwa sehemu kubwa Serikali wamejitahidi kuifanya kuwa bajeti ya kimkakati, sehemu mbalimbali ambayo wamefanya marekebisho ya kodi ni sehemu ambayo inasaidia kukuza na kulinda viwanda vya ndani” amesema Nape.

Nape ameongeza kuwa kama mapendekezo ya bajeti hiyo yatapitishwa, itasaidia kukuza na kuboresha maisha ya wananchi kwasababu moja ya vipaumbele vya bajeti hiyo ni katika suala la sekta ya kilimo.

Kwa upande mwingine Nape amedai kuwa kuna baadhi ya vipaumbele vya mapendekezo ya bajeti ambavyo bado kuna changamoto mathalani uwekezaji mkubwa kwa kutumia fedha za ndani katika miradi ambayo ingeweza kuwekezwa kibiashara.

Mbunge huyo ameitaka serikali kutanua wigo wa ukusanyaji kodi nchini ili kuweza kupunguza mzigo wa ulipaji kodi unaobebwa na wafanyakazi nchini na kudai kuwa, Tanzania ina takribani watu milioni 14 wenyesifa za kulipa kodi lakini wanaolipa kodi ni watu milioni 2.5 tu.


from MPEKUZI

Comments