Kocha wa Nigeria aeleza sababu za Kutandikwa Bao 2-0 Na Croatia Jana Usiku

Kocha ya kikosi cha timu ya taifa ya Nigeria, Gernot Rohr amesema kuwa makosa mengi waliyoyafanya katika mechi dhidi ya Croatia ni chanzo kikuu cha kipigo cha 2- 0 walichopokea.

Kikosi hicho maarufu kama ‘Super Eagles’ kilipokea kipigo hicho jana katika uwanja wa Kaliningrad nchini Urusi ambapo mchezaji wake Oghenekaro Etebo alijifunga na pia kupokea kipigo cha mkwaju wa penati uliopachikwa na Luka Modric.

“Tunafahamu kuwa tulifanya makosa mengi sana ambayo yalikuwa muhimu; na iko wazi kuwa tunatakiwa kuhakikisha tunayafanyia kazi ili twende mbele,” alisema kocha huyo.
 
Aliongeza kuwa kipigo hicho kimewavunja moyo wachezaji na kwamba wanapaswa kufanya kazi kiuweledi zaidi watakapokutana na vigogo wengine Argentina na Iceland.

“Tulijipanga vizuri na iko wazi kuwa mbinu zetu hazikuwa mbaya. Lakini tunatakiwa kuhakikisha tunazingatia weledi zaidi kabla ya michezo inayofuata,” aliongeza.

Aidha, kocha huyo ambaye amekiri kuwa kupoteza mchezo huo wa jana kunafanya kazi waliyoianza kuwa ngumu zaidi, alisema kuwa kiwango cha soka kilichooneshwa na nahodha wa timu hiyo Mikel Obi kilikuwa cha kuridhisha sawa na kiwango kilichooneshwa na safu ya ulinzi.


from MPEKUZI

Comments