CUF Upande wa Maalimu Wamtuhumu Msajili wa Vyama Kutaka Kumpa Fedha za Ruzuku Lipumba Kinyemela

Chama cha Wananchi (CUF) kimemwandikia barua Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Dar es Salaam kumtahadharisha kuwa Msajili wa vyama vya siasa Jaji Francis Mutungi anataka kuitumia benki  hiyo tawi la Zanzibar kuvunja kwa makusudi amri ya Mahakama kuu ya Tanzania.

Katika taarifa yao waliyoituma kwa vyombo vya habari jana  Juni 15, na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongofi ya CUF, Julius Mtatiro,  imedai Jaji Mutungi anataka kuitumia benki hiyo kuipa ruzuku CUF,  upande wa Ibrahim, Lipumba kwa kutumia bodi feki iliyosajiliwa na Rita Juni, 12, 2017.

Imesema bodi hiyo ilifungua akaunti Na. 22910021328 katika tawi la NMB Zanzibar na kuiandaa kwa matumizi ikihitajika.

“Huu ni ushahidi tosha kuwa njama na hujuma hizi dhidi ya CUF na demokrasia ya vyama vingi kupitia ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini zina baraka ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” imesema

Imesema Jaji Mutungi kwa sasa amepanga kuvunja amri hiyo kwa kutaka kutumia Benki ya NMB tawi la Zanzibar kwa kisingizio kuwa amri ya Mahakama Kuu ya Dar es Salaam haifanyi kazi na haina nguvu kisheria kwa upande wa Zanzibar.

“Ni matarajio yetu kuwa uongozi wa NMB utaendelea na msimamo wa kutii amri ya mahakama kuu na kuzuia kutolewa kwa fedha hizo. Ni imani yetu kuwa, kwa pamoja tutaweza kushirikiana katika kuhakikisha kuwa vita dhidi ya ukandamizwaji wa haki za kiraia zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria,” amesema Shaibu

“Kama chama tunapinga kwa pamoja ili haki hizo ziweze kutunzwa, kudumisha haki, uadilifu, amani na utulivu wa nchi yetu.” imesema


from MPEKUZI

Comments