Ajali Ya Basi Yaua Watano Geita

Watu watano wamefariki dunia na wengine 36 kujeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Mwanza kwenda Bukoba kupinduka.

Akizungumza leo Juni 17, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo amesema ajali hiyo iliyohusisha basi la King Msukuma na gari ndogo aina ya Harrier ilitokea jana asubuhi eneo la Kasamwa wilayani Geita.

Mabasi ya King Msukuma yanamilikiwa na mbunge wa Geita vijijini, (CCM) Joseph Kasheku maarufu kwa jina la Msukuma.

Kaimu Mganga Mfawidhi Hospitali ya Mkoa wa Geita, Dk Mazoea Fimbo amesema maiti za watu watano, wanawake wanne na mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi sita zimepokelewa na kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti hospitalini hapo.

"Majeruhi watatu wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi kutokana na hali zao kuwa mbaya na kuhitaji huduma Maalum," amesema Dk Fimbo.

Akizungumzia ajali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel amesema kwa mujibu wa maelezo ya mashuhuda, ajali hiyo ilitokea baada ya basi kukosa mwelekeo na kulifuata gari dogo upande wa kulia wa barabara na kuligonga ubavuni kabla ya magari yote mawili kupinduka.


from MPEKUZI

Comments