Wanahisa Wamgomea Dk Kimei .....Wataka Asiondoke CRDB

Baadhi ya wajumbe waliohudhuria mkutano mkuu wa mwaka wa Benki ya CRDB unaofanyika leo Mei 19, 2018 jijini hapa, wamemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Dk Charles Kimei kuendelea kuitumikia benki hiyo.

Kauli za wanahisa hao waliohudhuria mkutano mkuu wa 23 wameeleza hayo baada ya Dk Kimei kuwajulisha kuwa kwenye mkutano mkuu ujao, atawaaga rasmi.

"Hotuba yangu ya leo si ya mwisho. Tutakutana tena mwakani nitakapowaaga. Mkataba wangu unaisha Mei, 2019,” amesema  Dk Kimei alipokuwa akitoa hotuba ya mwenendo wa benki hiyo ambayo mwaka 2017 imepata faida ya Sh36 bilioni ambayo imepungua kutoka Sh70 bilioni iliyopata mwaka 2016.

Kwenye michango yao, baadhi ya wanahisa hao wamesema kipindi hiki ni kigumu kiuchumi hivyo CRDB inahitaji mtu mwenye uzoefu wa kutosha kukabiliana na changamoto zilizopo.

Mmoja wa wanahisa hao, Lemburis Sirikwa (76) wa Arusha amesema endapo mkurugenzi huyo ataondoka na kuiacha benki hiyo, ndani ya miaka miwili ya kutokuwa naye lazima ufanisi utapungua.

"Kimei shall remain until further notice (aendelee kuwepo mpaka taarifa nyingine itakapotolewa). Kama bodi haitaki kufanya hivyo, tutachagua wajumbe wengine," amesema Sirikwa.

Sirikwa amesema wapo wakurugenzi wenye umri wa miaka 90 lakini wanaendelea kuziongoza taasisi zao hivyo haoni sababu ya Kimei kustaafu.

"Kimei ni mdogo sana. Mimi nina miaka 76, namzidi mbali sana. Asiondoke sasa hivi," amesema.

Mwanahisa mwingine kutoka mjini Sumbawanga, Kapteni mstaafu Noel Nkoswe amesema suala la kumpata mkurugenzi ni gumu.

"Tulipoanza, tulitafuta mtu anayefaa lakini hatukupata. Mwishowe tukaenda kuiomba  Benki Kuu ambayo ilitupatia Dk Kimei. Tunaishukuru Benki Kuu kwa kutupa mtaalamu huyu, napendekeza aendelee kuwepo walau miaka miwili au mitatu zaidi," amesema.


from MPEKUZI

Comments