Tochi Za Trafiki Pwani Zakaguliwa Ubora Wake

Wakala wa Vipimo Tanzania  (WMA),  umekagua vifaa vya kubidhiti mwendo maarufu kama tochi zinazotumiwa na Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, kuhakiki ubora wake.

WMA imefanya ukaguzi huo mapema leo katika Mkoa wa Pwani ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani ambayo hufanyika Mei 20, kila mwaka.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ukaguzi huo Mkurugenzi wa Ufundi wa WMA Tanzania, Stella Kahwa amesema hatua hiyo imelenga pia kuhakiki usalama wa vifaa hivyo katika kudhibiti mwendo.

“WMA hapo awali tulikuwa tunapima ubora wa vipimo kama vile mizani lakini sasa tumeendelea kuongeza wigo wa kazi zetu tunapima vipimo vya sekta ya biashara,  afya na mazingira,” amesema.

Amewahakikishia watumiaji wa barabara hususan madereva wasiwe na wasiwasi kwani ubora wa vifaa hivyo ni wa uhakika.

“Wawe makini wanapokuwa barabarani kwa sababu akienda mwendo wowote uwe kasi ama la, kifaa hiki kinaweka taarifa zake, ukienda speed 70 ni 70 na kama ni 80 kinaonesha hivyo hivyo 80 ” amesema.

Naye, Mrakibu wa Polisi na Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Makao Makuu, Abel Swai amewahimiza madereva kuendelea kuzingatia na kutii sheria za usalama barabarani.


from MPEKUZI

Comments