Swali La Kwanza Alilouliza SUGU Leo Bungeni

Leo May 21, 2018 Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amesimama na kuuliza swali Bungeni kwa mara ya kwanza tangu atoke gerezani Ruanda, Mbeya May 10 alipokuwa akitumikia kifungo cha miezi mitano.

Sugu aliuliza swali lake mara baada ya Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa  kujibu swali la msingi la  Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea (Chadema) lililohusu sheria za makosa ya mtandao.

Mwenyekiti wa Bunge, Chenge alimruhusu Sugu aulize swali la nyongeza ambapo alisema: “Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti, niwatakie mfungo mwema ndugu zangu Waislamu, ndani ya bunge na nchi nzima kwa wale ambao ni viongozi wautumie mwezi huu kujitathmini.

Kutokana na maelezo hayo ya Sugu, Chenge alimkatisha Sugu na kumtaka kuuliza swali moja kwa moja.

Sugu aliendelea kwa kusema: “Sheria hii pamoja na sheria nyingine mbovu za habari si tu zinawabana wananchi kupata habari bali zinatumika pia kufunga watu jela hovyo kisiasa…

“Mfano mimi nilifungwa kwa kujadilina na wananchi wangu taarifa za watu kupigwa risasi, watu kutekwa, maiti kuokotwa kwenye viroba, watu kutokuwa na uhuru wa kuongea….

Chenge alimkatisha Sugu kwa mara ya pili akimtaka kuuliza swali: “Mheshimiwa uliza swali.”

Sugu aliendelea: “Kitu ambacho si mimi tu najadili kwani kilishajadiliwa  ndani ya Bunge hili na pia Maaskofu wa Katoliki…

Chenge aliingilia tena: “Uliza swali,Uliza swali Mheshimiwa, hapana, hapana sina muda, uliza swali.”

Sugu: “Ni lini sheria hizi zitafutwa ili kulinda Katiba ya hususani Ibara ya 18 mfano maslahi  mapana ya demokrasia  nchini,”.

Chenge alimkatisha kwa kumwambia; “umeeleweka Mheshimiwa…”

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na  Mawasiliano, Kwandikwa alitumia muda huo kumkaribisha Mbunge huyo bungeni kwa mara nyingine.

“Kwanza nimkaribishe Mheshimiwa Sugu ndani ya nyumba Mheshimiwa karibu sana, lakini napenda kumjibu kuwa sheria zote Serikali inazitazama, na kama kuna maeneo yanahitajika marekebisho hufanya hivyo mara moja kwa kutumia Bunge.

“Labda kama kuna eneo mahususi kwa sababu Mheshimiwa Sugu umekuja tuonane ili na mimi nipate kwa upana kile ambacho unakizungumza, halafu sisi baadaye kama Serikali tutaangalia kwa nia nzuri ili sheria bora zaidi,” amesema.


from MPEKUZI

Comments