Makonda ayakana makontena Yaliyoko Bandarini

Utata umeendelea kuandama umiliki wa makontena 20 yaliyotajwa na Mamlaka ya Mapato (TRA), kuwa miongoni mwa yale yatakayopigwa mnada kwa kukaa bandarini muda mrefu, baada ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kukana kuwa sio ya kwake.

Awali, TRA ilitoa tangazo katika gazeti la Daily News, ikisema mtu aitwaye Paul Makonda bila kubainisha kama mtajwa ni mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam au la, anamiliki makontena 20 yenye bidhaa mbalimbali zikiwamo samani katika bandari kavu ya DICD.

Hata hivyo, akizungumza jana wakati akizindua kamati ya mapendekezo kuhusu wanawake waliotelekezwa na wenza wao, Makonda alisema hajui chochote na amesikia habari hizo kwenye magazeti kama walivyozisikia watu wengine.

“Sidhani kama nahusika na jambo lolote lile na sijui chochote, hilo unalolisema hata mimi nimesoma kwenye magazeti kama ulivyosoma wewe. Nafikiri zilikuwa ni habari za jana na leo nimesoma nyingine,” alisema.

Makonda alisema Serikali hufanya kazi zake kwa maandishi na yeye hana nakala yoyote inayohusiana na mzigo huo.

“Sio suala la kwangu kabisa, nimekusikia wewe kama mimi nilivyosikia jana (juzi) na ninafikiri tutaendelea kusikia hivyo hivyo na ndio maana katika hizo habari hakuna sehemu yoyote umeona nimenukuliwa kusema kama ni mali zangu,” alisema Makonda.

Hata hivyo, Februari 16, Makonda alikaririwa na  gazeti la Serikali la HabariLeo kuwa alipokea makontena 20 yenye samani zitakazotumika katika ofisi za walimu zinazoendelea kujengwa ukiwa ni sehemu ya shehena ya makontena 36.

Ilielezwa kuwa samani hizo za ofisini zilizokuwa na thamani ya Sh2 bilioni, zilitolewa na Watanzania wanaoishi Marekani wanaojulikana kama Six Region Diaspora Council.

Mei, 12 kaimu kamishna wa Forodha na Ushuru wa TRA, Ben Asubisye alisema wamiliki wa mizigo hiyo wanatakiwa kuikomboa ndani ya siku 30 kuanzia siku hiyo. Katika tangazo hilo lenye orodha ya makontena zaidi ya 800, jina la Paul Makonda limejitokeza mara 20 akiwa mpokeaji wa makontena 20 yakiwa na bidhaa kadhaa, zikiwamo samani.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema juzi kuwa mamlaka hiyo imetoa notisi ya siku 30 kwa waagizaji wa mizigo ambayo imekaa bandarini kwa zaidi ya siku 90.

“Tangazo lililotolewa ni notice (taarifa) kwa wahusika ili wakomboe mizigo yao ndani ya siku 30. Isipokombolewa itanadiwa. Mizigo hiyo inaweza kuwa ni ile ambayo haijalipiwa kodi au hata ile iliyolipiwa lakini haijaondolewa,” alisema.

Alipoulizwa kama shehena hiyo ni mali binafsi ya Makonda au ya ofisi yake, Kayombo alisema: “Majina yaliyoandikwa kwenye magazeti ndiyo taarifa za consignees (wapokeaji) zilizopo kwenye nyaraka.”


from MPEKUZI

Comments