Serikali Yagoma Kurejesha Ardhi kwa Wananchi

Serikali imesema haina mpango wa kurejesha kwa wananchi eneo la ardhi katika Gereza la Matongo kama ilivyoombwa na Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema leo Aprili 19 bungeni na kueleza kuwa  gereza hilo lililopo mkoani Simiyu katika Wilaya ya Bariadi lenye ukubwa wa eka 2,472.62 bado lina umuhimu wake hasa katika shughuli za kilimo.

Masauni amesema gereza hilo lilianzishwa mwaka 1975 kwa kuchukua eneo lililokuwa la mbunge wa zamani wa Bariadi, Edward Ng'wani (marehemu) ambaye alifidiwa eneo jingine la Serikali.

"Gereza la Matongo lililopo mkoani Simiyu katika wilaya ya Bariadi lenye ukubwa wa ekari 2472 lilianzishwa mwaka 1975, baada ya kuchukuliwa eneo hilo lililokuwa eneo la Mbunge wa enzi hizo Edward Mwani ambaye alifidiwa eneo jingine na serikali. 

"Kwa serikali ipo kwenye mpango wa kuboresha kilimo kupitia jeshi la magereza kwa kuliwezesha kuzalisha chakula cha kutosheleza kulisha wafungwa na mahabusu hivyo eneo la Matongo lipo kwenye orodha ya maeneo yaliyopewa kipaumbele katika kilimo cha mahindi, alizeti, pamba, ufugaji wa nyuki na mifugo pamoja na upandaji wa miti na uhifadhi wa mazingira, 

"Serikali ilichukua eneo hilo ili kuwezesha magereza kuendeleza shughuli za uelimishaji wa wafungwa kwa kutumia kilimo na ufugaji kwa sasa eneo hili limepimwa na taratibu za kupatikana kwa hati zinaendelea hivyo serikali haina mpango wa kurejesha eneo hilo kwa vijiji tajwa" alisisitiza Masauni

Majibu ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni yalimuinua tena Andrew Chenge na kutaka kufahamu ni lini serikali itakuwa tayari kuanza mpango huo kwani ni miaka mingi imeshindwa kufanya hivyo. 

"Mhe. Spika gereza na Matongo ni gereza ambalo ni miongoni mwa magareza yaliyoanzishwa na serikali katikati ya miaka ya 70 kwa lengo hilo hilo ambalo waziri amelisema lakini zaidi ya miaka 40 ukifika pale Matongo hakuna cha maana kinachoendelea na Mhe.

"Waziri katika majibu yake anasema gereza hili lipo kwenye mpango wa kuboresha kilimo sasa ni lini mpango huu mahususi kwa gereza la Matongo utaanza kutekelezwa na serikali" alihoji Andrew Chenge 

Awali, Chenge aliiomba Serikali kama itakuwa tayari kurejesha eneo la gereza hilo kwa wananchi wa vijiji vinavyolizunguka.

Naibu Waziri Masauni amesema wananchi wa vijiji vya Mwanchumu na Salaliya kwa asili yao si wenyeji, bali ni wahamiaji kutoka maeneo mengine.

Amesema Serikali ilitwaa eneo hilo ili kuliwezesha Jeshi la Magereza kuendeleza shughuli za urekebishaji tabia wafungwa na mahabusu.


from MPEKUZI

Comments