Serikali Yaeleza Utekelezaji Hoja Za CAG Sekta Za Afya Na Elimu

Serikali imesisitiza kuwa hakuna hoja ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika sekta zote na hususani sekta za Afya na Elimu ambayo haitatekelezwa ili kuhakikisha azma ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafikiwa ipasavyo.

Ahadi hiyo imetolewa mjini hapa leo na Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia walipozungumza na waandishi wa habari kueleza utekelezaji wa hoja za CAG katika sekta zao.

Waziri Ummy: Tunakagua Deni la Wagonjwa Nje
Akieleza utekelezaji wa hoja mbalimbali katika sekta ya Afya, Waziri Ummy ameeleza kuwa Wizara ya Afya, baada ya kupata taarifa ya CAG kuhusu kuongezeka kwa deni la matibabu ya wagonjwa wanaopata rufaa nje ya nchi, imeamua kufanya uchunguzi wa kina wa kitabibu na kihasibu kujua usahihi wa deni hili ili kuchukua hatua madhubuti.

Aidha, amesisitiza kuwa Wizara imekubaliana na ushauri wa CAG wa kuhakikisha Serikali inaendelea kuboresha utoaji wa huduma za kibingwa hapa hapa nchini nchini ili kupunguza gharama. Waziri Ummy ameeleza hatua mbalimbali zilizochukulia kutekeleza agizo hilo ikiwemo kuanza kutolewa hapa nchini huduma za upasuaji wa moyo, upandikizaji wa figo, uwekaji wa vifaa vya usikivu na matibabu ya magonjwa ya mifupa na mishipa ya fahamu.

Kwa upande wa huduma za kibingwa katika maradhi ya saratani, Waziri Ummy alisema tatizo kubwa lililopo sasa ni huduma za kiwango cha juu cha kupima ugonjwa huo ambazo hazipatikani sehemu nyingi za Afrika. Hata hivyo alisema katika mwaka mmoja ujao Tanzania itamaliza tatizo hilo kwani Serikali imetenga Shilingi bilioni 14.5 mwaka ujao wa fedha kununua mashine ya kupima saratani (PET-CT-SCAN)

Kuhusu uingizwaji wa bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 1.94 kwa kutumia vibali vya kughushi, Waziri Ummy amesema wameshachukua hatua za haraka kupitia Bodi ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kuwabaini wote waliohusika na tayari baadhi wameshakabidhiwa kwenye vyombo vya dola huku TFDA ikichukua hatua za kujiunga na mfumo wa TRA ili kutambua nyaraka zisizo halali.

“Wizara yangu itahakikisha kuwa maoni yote ya CAG yanaendelea kufanyiwa kazi kwa haraka zaidi ili kuhakikisha hakuna senti ya wananchi katika sekta ya afya inatumika kinyume na matarajio,” alisema Waziri Ummy.

Prof. Ndalichako: Tunakichunguza Kitengo cha Manunuzi
Akizungumzia maeneo kadhaa ya sekta ya elimu, Waziri Ndalichako amekubaliana na hoja mbalimbali za CAG hasa katika eneo la ucheleweshaji wa ujenzi wa miradi mbalimbali ya elimu ikiwemo ucheleweshaji wa mradi wa ujenzi wa shilingi bilioni 4.6 katika Chuo cha Ualimu Ndala.

Prof. Ndalichako amekiri kuwa kuna tatizo ndani ya Kitengo cha Manunuzi wizarani kwake. Kufuatia hali hiyo, ameagiza uchunguzi kuhusu ufanisi wa Kitengo hicho ambao utakamilika mwishoni mwa mwezi huu na amesisitiza kuwa hatasita kuchukua hatua kali dhidi ya watakaobainika kuchelewesha miradi muhimu ya maendeleo.

Kwa upande wa changamoto mbalimbali katika utoaji na ufuatiliaji wa madeni ya mikopo ya Elimu ya Juu, Prof. Ndalichako ameeleza hatua mbalimbali ambazo Serikali imezichukua ikiwemo kuteua Mkurugenzi Mkuu mpya wa Bodi ya Mikopo na kuunda Bodi mpya Agosti mwaka jana; mabadiliko ambayo yameleta mageuzi katika kupunguza muda wa wanafunzi kupata mikopo na vile vile kuongezeka makusanyo ya madeni ya mikopo.

“CAG alionesha kuwa miaka ya nyuma Bodi ilikuwa inakusanya kati ya Shilingi bilioni 32 na 48 za madeni ya mikopo. Lakini tangu iingie Serikali ya Awamu ya Tano na mabadiliko yaliyofanyika, ukusanyaji umeongezeka hadi shilingi bilioni 116 mwaka 2016/17 na mwaka huu wa fedha hadi kufikia Machi, 2018 kiasi cha Shilingi bilioni 132.20 ambazo ni sawa na asilimia 101 ya lengo la mwaka 2017/18,” alisema na kuongeza:

“Nakiri pia kwamba huko nyuma kulikuwa na udhaifu katika kuwatambua wadaiwa sugu. Hivi sasa kazi inafanyika ambapo Bodi ya Mikopo imeongeza idadi ya kuwatambua wadaiwa sugu kufikia 147,231 mwaka 2017/18 kutoka wadaiwa sugu 48 tu waliobainishwa awali ambapo kati ya waliobainishwa jumla ya wadaiwa 42,213 wameshaanza kulipa madeni yao ya mikopo.”

Waziri Ndalichako ametumia fursa hiyo kusisitiza kuwa Wizara yake pia imewaagiza wataalamu na viongozi wote wa taasisi zilizo chini yake kuhakikisha kuwa wanapitia neno kwa neno taarifa ya CAG ili kuhakikisha maeneo yote yenye changamoto yanafanyiwa kazi.

Kesho katika mfululizo wa mawaziri kueleza utekelezaji wa hoja za CAG itakuwa ni zamu ya Wizara ya Nchi (Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira) na Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi,
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.


from MPEKUZI

Comments