Serikali Kumwaga Ajira 25,000 kwa watumishi wa kada ya afya

Serikali imepanga kuajiri watumishi wa kada ya afya wapatao 25,000 katika mwaka wa fedha 2018/19.

Kauli hiyo imetolewa bungeni mjini Dodoma leo Jumatatu Aprili 23, na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Josephat Kandege wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbulu Mjini, Zacharia Issay (CCM).

Katika swali la msingi Issay alitaka kujua serikali ina mkakati gani wa kuongeza watumishi katika Hosptali ya Wilaya ya Mbulu ambapo Kandege amesema tayari Tamisemi imeomba kibali cha kuajiri watumishi wa kada ya afya 25,000 ili kuhakikisha kunakuwapo na watumishi wenye sifa stahiki kwenye hospitali, vituo vyote vya afya na zahanati.

“Serikali inaendelea na ujenzi wa vituo vya afya 208 nchi nzima ili kuboresha huduna ya dharura kwa mama wajawazito, ujenzi wa vituo hivyo utagharimu Sh bilioni 132.9 hadi kukamilika.

“Sambamba na ujenzi huo, vituo hivyo vimetengewa Sh bilioni 35.7 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba ili kuviwezesha kutoa huduma kwa wagonjwa,” amesema.


from MPEKUZI

Comments