Polepole Amvaa Zitto Kabwe Kwa Madai Kuwa Anapotosha Kuhusu Ripoti ya CAG

Katibu wa Halmashauri Kuu Itikadi na Uenezi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Humphrey PolePole amefunguka na kuwavaa viongozi ambao wanazungumza juu ya ripoti ya CAG na kusema baadhi ya viongozi hao wanapotosha Umma kwa kusema mambo ya uongo.

Polepole amesema hayo leo April 18, 2018 wakati akiongea na waandishi wa habari na kusema wapo viongozi wa vyama vya siasa hawazungumzi juu ya mambo mazuri yaliyofanywa na serikali kama ujenzi wa miundombinu na mambo wanayopiga hatua ila wamekuwa wakidakia mambo na kutoa taarifa za uongo.

"Sasa unaposoma taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) halafu unatoa kauli timilifu kuwa pesa imeibiwa, yaani pesa ya Umma imeibiwa. Tunaweza tukakwambia tusaidie kuthibitisha sasa ukishindwa umesema uongo umeuhadaa Umma, umetoa takwimu za uongo ukichukuliwa hatua sio ndiyo utaanza kusema uongozi huu hatuna huruma, huruma kwa watu waovu? Waongo wanaopotosha kwa makusudi hilo halikubaliki".Amesema Polepole

Akaendelea kusema, "Mimi sielewi huyu anayekwenda mbele kusema taarifa za uongo uongo hivi, ndiyo mtaji wake siku hizi anatafuta tu pahala. hoja hana, hazungumzi kuhusu rushwa siku hizi, hazungumzi kuhusu huduma za kijami, hazungumzi kuhusu ufisadi, hazungumzi kuhusu miundombinu, tunapiga hatua kubwa, tunapeleka watoto shule bure, bali yeye anatafuta hoja ya uongo uongo" alisema Polepole

Polepole katika mkutano huu ameeendelea kumtuhumu mtu huyo kushindwa kuwa na uhakiki wa maneno yake

"Kuna kipindi mtu huyu alizungumza kuhusu njaa, wewe unaijua njaa inatangazwa vipi sasa tumevumilia sana leo tumeshindwa tumeona tumsaidie kumuelewesha halafu tuseme wale ambao wana dhamana ya kuhakiki maneno tunayatoa kwa kweli wachukue hatua kwani hatupo tayari kuacha watu wachache waendelee kuudanganya umma wa watanzania hili halikubaliki" alisisitiza

Mwisho wa wiki iliyopita, Mbunge wa Kigoma Mjini kwa triketi ya ACT Wazalendo, Zitto Kabwe aliizungumzia kwa mapana zaidi taarifa ya CAG na kuonyesha mambo ambayo serikali imetuhumiwa kufanya ikiwa pamoja na upotevu wa fedha zaidi ya Trilioni 1.5 ambayo haina maelezo imetumikaje.


from MPEKUZI

Comments