Baba aondoka na mtoto wa Masogange siku moja ya mazishi

Ikiwa ni siku moja tangu msanii Agnes Gerald ‘Masogange’ azikwe, mtoto wake wa pekee Sania Sabri ameondoka na baba yake kurudi jijini Dar es Salaam.

Marehemu Masogange alizikwa jana Aprili 23 mwaka huu pembeni mwa nyumba ya baba yake, Gerald Waya katika kijiji cha Utengule, Mbalizi II mkoani Mbeya.

Baba wa marehemu, Waya amesema mjukuu wake, Sania ameondoka leo Aprili 24 na baba yake Sabri Athman kuelekea jijini Dar es Salaam, ili kuwahi masomo  kwa kuwa sasa hakuna shughuli yoyote ya familia.

Amesema licha ya kumfahamu mjukuu wake Sania, hakuwahi kumfahamu baba yake hivyo msiba huo ndiyo uliowakutanisha na kufahamiana kwa mara ya kwanza. 

 “Mjukuu wangu Sania ameondoka leo alfajiri na baba yake. Sababu ni kuwahi masomo shuleni kwani tumeona shughuli zote ziliisha jana hakuna sababu ya kuendelea kuwa naye hapa, atakuja wakati wa kumaliza matanga,” amesema.

Waya amesema shughuli za kuondoa matanga zitafanyika baada ya siku 40 kupita na  jana walifanya shughuli ya kuwaaga waombolezaji waliolala msibani hapo na kubakia familia tu.

“Hivi sasa kama unavyoona hakuna kinachoendelea, tumebaki familia tu ambayo tutaendelea kuomboleza hadi baada ya siku 40 ya matanga. Haitafanyikia hapa nyumbani badala yake tutarudi kule nyumbani asili ambako ndiko kuna makaburi ya ukoo na nyumba ya baba yangu ipo kule,” amesema  Waya.

Amesema familia zao zote huzikwa kwenye makaburi hayo, lakini mtoto wake ameamua azikwe pembezoni mwa nyumba yake ili asikae mbali naye. Pia, kwenye makaburi ya pamoja kwa sasa hapapitiki kwa urahisi kutokana na mvua zinazoendelea.


from MPEKUZI

Comments