Wazee CHADEMA Waomba Kukutana na Rais Magufuli

Baraza la Wazee wa Chadema limemuomba Rais John Magufuli kukutana na  wazee ili kubadilishana nao mawazo sambamba na kumpa ushauri wa masuala mbalimbali yanayoendelea nchini.

Akizungumza leo Jumanne Machi 13, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, katibu mkuu wa baraza hilo, Roderick Lutembeka amesema kumekuwa na mambo mengi yanayopigiwa kelele, ni vyema rais akakutana na wazee ili wamueleza mambo hayo.

“Ni lazima kama Taifa tuchukue hatua mapema kabla hatujachelewa. Rais Magufuli akubali kuitikia wito wa kukutana na wazee ambao watakuwa na ujasiri wa kumshauri ili kuepusha Taifa kuingia kwenye majanga,” amesema.

Amesema suala la wazee kukutana na rais, kimekuwa ni kilio cha muda mrefu na kwamba nchini Kenya viongozi wameweza kukaa meza moja na kumaliza tofauti zao.

“Lazima tukae tujue mustakabali wa Taifa hatuwezi kusema hakuna tatizo. Tunamtaka akutane na wazee, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa tuzungumze kwa kuwa hii ni nchi yetu wote na si ya chama kimoja,” amesema.

Amesema mambo yanayopaswa kuzungumziwa ni suala la Katiba Mpya, hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Amesema pia matukio ya watu kutekwa na kuuawa yameongezeka, “miezi sita iliyopita tulizungumzia mambo haya lakini naona ndio yanaongezeka.”

“Wazee tumeumizwa mno kuhusu suala la Abdul Nondo hasa pale Waziri wa Mambo ya Ndani (Mwigulu Nchemba) alipotoa kauli kuwa kijana huyu alijiteka. Tulitegemea polisi wafanye uchunguzi, sasa kama waziri mhusika tayari ameshatoa hukumu tutegemee nini kwa hawa polisi. Tunajenga nini ndani ya mioyo ya hawa vijana ambao walijitoa kumtetea kijana mwenzao kama si chuki.”


from MPEKUZI

Comments