Rais Magufuli Na Maendeleo Ya Viwango Vya Olimpiki

Na Judith Mhina-MAELEZO
Uzinduzi wa tawi la CRDB Chato uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli unadhihirisha Tanzania ya maendeleo ni lazima.

“Kujenga standard gauge kwa shilingi trilioni 7.6 fedha za ndani, msifikiri watu wanafurahi” 

“Tunapoamua kujenga Stigler’s Gorge ambayo itazalisha umeme zaidi ya megawati 2100 usifikiri wanaweza kufurahi” 

”Tunapoweza kununua ndege kwa fedha zetu, kitu ambacho tulishindwa kwa miaka 50 usifikiri watu wanafurahi” 

“Tunapoweza kulipa mishahara tarehe 21 usifikiri wengine wanafurahi”. Rais Magufuli.

Maneno hayo ya Rais yametokana na utekelezaji wa miradi mikubwa kadhaa ya maendeleo, kupiga vita rushwa, uboreshaji wa huduma za jamii hususan elimu bure, afya, usambazaji wa umeme, maji na matumizi sahihi ya fedha za Umma zimeipaisha Tanzania kiuchumi.

Nina hakika sio rahisi kumshawishi Mwingereza au nchi yeyote iliyobobea kwenye uchumi mkubwa iwapo unafanya hovyo hovyo, eti akushabikie kuwa nchi yako uchumi wake unamuelekeo mzuri na itafika mbali. Lakini leo sio ajabu maana imetokea Tanzania ambayo ina muelekeo mzuri wa uchumi na inatabiriwa kufika mbali kimaendeleo.

Penye ukweli uongo hujitenga, Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika nchini Uingereza Stewart Rory ameeleza namna alivyovutiwa na mabadiliko yanayofanywa kwenye sekta ya elimu, kupitia sera ya elimu bure ambayo imewezesha kuwepo kwa ongezeko kubwa la udahili wa wanafunzi.

Kufuatia mabadiliko hayo Uingereza imetoa Paundi milioni 140 kusaidia maboresho katika miundombinu ya utoaji wa elimu hususan ujenzi wa madarasa na nyenzo za ufundishaji.

 “Nimetembelea shule za msingi na kushuhudia mabadiliko makubwa yaliyofanyika, ikiwemo utoaji elimu bure. Tutatoa zaidi misaada kusaidia masuala ya kitaaluma, ikiwemo ujenzi wa madarasa”. Amesema Rory.

Aidha, Balozi wa ufaransa nchini Friederic Clavier alipokwenda kumtembelea Mhe. Samia Suluhu Hassan Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ofisini kwake Jijini Dar-es-salaam, alisema kuwa, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, anaunga mkono juhudi za dhati zinazochukuliwa kuhakikisha uchumi wa Tanzania unaimarika.

“Rais wa Ufaransa anauhakika na Tanzania ijayo na anaunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanywa na Rais Magufuli” amesema Clavier.

Naye, Muwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kwenye masuala ya Watoto Profesa Virginia Gamba amesema kuwa anaipongeza Tanzania kwa jitihada za kudumisha amani ndani na nje ya nchi.

Aidha, amesema;“Tanzania ni miongoni mwa nchi ya kuigwa Afrika zinazopiga hatua kubwa ya maendeleo zinazopaswa kutiliwa mfano lakini yote hiyo inatokana na umadhubuti wa serikali yake na Jeshi la Wananchi wa Tanzania”.

Pia, Muwakilishi wa Benki ya Dunia katika nchi za Burundi, Malawi na Somalia Bibi Bella Bird tarehe 4 Desemba mwaka jana akiwa Ikulu Jijini Dar-es-salaam, alimuhakikishia Rais Magufuli kuwa taasisi hiyo, imejipanga kuendelea kutoa mikopo nafuu kwa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini. Hii yote ni kwa sababu ya usimamizi mzuri wa fedha za maendeleo ambazo zinasimamiwa na serikali ya Rais John Pombe Magufuli

Bibi Bird amesema “2016 Benki ya dunia ilitoa mkopo nafuu yenye dhamani za Dola ya Marekani bilioni 1.2, ambazo zilikuwa sawa na trilioni 2.7 fedha ya Tanzania. Fedha hizi zimekwenda katika miradi mbalimbali na tunafurahi kuwa zimetumika vizuri kama ilivyokusudiwa’

Benki ya Dunia imetoa kipaumbele katika miradi ya miundombinu ya barabara na reli, kuongeza usambazaji na uzalishaji wa nishati ya umeme, tekinolojia ya habari na mwasiliano,  elimu, ili kuhakikisha idadi ya wanaopata elimu inaongezeka, uboreshaji wa sekta ya afya,  na kuongeza upatikanaji wa maji safi.

Akizungumzia hali ya uchumi Wilayani Chato Rais Magufuli amesema;”Kwa sasa tupo kwenye mstari sahihi nawaomba Watanzania mvumilie ili tufike mahali ambako Tanzania itakuwa nchi ya asali”

Rais Magufuli anamaanisha kuwa, Tanzania itakuwa nchi ya asali kweli kutokana na mbio, kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano hii ni dhahiri bila kificho. Mpaka sasa kila kitu cha maendeleo kinachofanywa na Serikali kinawekwa hadharani ili kudhihirisha imedhamiria kutenda inachosema.

“Niliapa kwa Katiba kwamba nchi hii lazima iwe ya amani nataka tujenge uchumi wa kweli” amesema Rais Magufuli.

Haiingii akilini nje ya Tanzania watu wanaona mbio za maendeleo zinavyoshika kasi hapa nchini, na kutabiri matokeo yake kuwa ni ustawi wa nchi na watu wake. Lakini ndani ya Tanzania waone ni mateso, kutoa maneno yasiyofaa na kutaka kufanya vitu vinavyovuruga amani, upendo na mshikamano jambo hili tulikatae.

Vilevile, Rais aliongeza kuwa Tanzania ya viwanda imeanza kupatikana na kinachohitajika ni kuongeza juhudi bila kujali vitisho na maneno ya kukatisha tamaa kutoka kwa yeyote ndani au nje ya nchi.

 “Tunaposema viwanda kuna mataifa yahapendi. Hata tukitaka kujenga viwanda vya nguo hawataki kwa sababu wananufaika. Wanataka tulime Pamba kisha tuwauzie wao watengeneze nguo kisha wazivae halafu watuletee mitumba”. Amesema Rais Magufuli

Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya madini, Royalty Exploration Corporation (TRX) kutoka Canada James Sinclair amesema; “Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli amekaribisha wawekezaji zaidi baada ya kupiga vita rushwa na udanganyifu katika mfumo”. 

Aidha, Sinclair aliongeza kwa kusema kuwa, Serikali imeweka mazingira mazuri ya kiuchumi na kisiasa kuhusu uwekezaji nchini Tanzania. Ambapo kampuni yake imeingia makubaliano na Wakala wa Madini Tanzania (STAMICO) miaka kadhaa iliyopita, lakini haikuathiriwa na mabadiliko ya sheria, kwa kuwa walishaingia katika mabadiliko ya ulipaji wa kodi. 

Akizungumzia suala la viwanda wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha sigara cha Philip Moris Tanzania Ltd, kilichopo mjini Morogoro, Rais amekuwa mwalimu mzuri na kutoa somo kwa Watanzania kuwa kiongozi mzuri ni yule anayetatua kero na sio anayetengeneza kero.

“Serikali imejifunza kutokana na makosa ya hapo nyuma ya kuweka kodi kubwa kwenye  viwanda ambapo ilisababisha viwanda vingi kufa, sasa mazingira mazuri yanawekwa ili kulinda viwanda hivyo”; amesema Rais Magufuli

Kitendo ambacho kinashawishi wawekezaji wengi kuja Tanzania kuwekeza pamoja na wazawa kama alivyofanya Philip Moris Tanzania Ltd na Mansoor, au kiwanda cha sukari kinachotarajiwa kuzinduliwa ambacho kinajengwa  na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Tumuunge mkono Rais kwa kila jambo analotekeleza ili tuende sote kwa pamoja, tuweze kutumia fursa mbalimbali za kazi, biashara na uwepo wa soko la uhakika la Afrika Mashariki lenye idadi ya watu takribani milioni 200. Pia, soko lipo la Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) 665.

Mafanikio yote hayo yametokana na usimamizi mzuri wa matumizi ya fedha za umma kwenye wa miradi mikubwa ya maendeleo ambayo ni gumzo ndani na nje ya Tanzania. 

Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa reli ya kisasa unaojengwa kwa fedha za ndani ni mfano wa kuigwa  Barani Afrika, Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga  na mradi wa Umeme wa Stiglers Gorge wa Rufiji.

Miradi mingine ni ununuzi wa ndege 6, ujenzi wa kiwanda cha kimiminika cha gesi Mkoa wa Lindi, Mpango wa Elimu Bure, Mabasi ya mwendo kasi na Tanzania ya viwanda kila Mkoa viwanda 100. 

Aidha ujenzi wa meli katika ziwa Nyasa, Victoria na Tanganyika, Mpango wa umeme Kinyerezi 11, 111, usambazaji wa umeme vijijini, upanuzi wa viwanja vya ndege na vita dhidi ya rushwa.


from MPEKUZI

Comments