NACTE yavifungia udahili vyuo 163


 Baraza la Taifa la Elimu na Ufundi (Nacte) limezuia vyuo 163 kudahili wanafunzi katika kozi mbalimbali ngazi ya astashahada na shahada, baada ya kukutwa na upungufu ikiwako kutokuwa na walimu wenye sifa.

Akizungumza leo, Machi 23 na waandishi wa habari, Mkuu wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Nacte, DK Annastella Sigwejo amesema walifanya uhakiki kwa vyuo 459, kati ya hivyo 296 ndivyo vimekidhi vigezo vya kutoa elimu kwa kiwango kinachotakiwa.

"Kutokana na hali hiyo hivyo ndivyo vinaruhusiwa kudahili wanafunzi kwa ajili ya kozi mbalimbali ngazi ya astashahada na stashahada kwa muhula wa udahili wa Machi na Aprili mwaka huu.”

Amesema licha ya kwamba vyuo vilivyosajiliwa viko 580 waliamua kujiridhisha kwa kuvifanyia uhakiki ambapo walifanikiwa kuhakiki vyuo 459.

Nacte wanawashauri wanafunzi kuhakikisha wanajiridhisha kuwa wanaomba kujiunga kwenye vyuo vilivyokidhi vigezo.

Mkuu wa Kitengo cha Udahili, Twaha Twaha amesema kuwa majina ya vyuo vilivyoruhusiwa kudahili yamewekwa kwenye tovuti ya Nacte.

"Hivyo Nacte inashauri waombaji wa udahili kujiridhisha kwa kuangalia hiyo orodha iwapo chuo anachokitaka kinaruhusiwa kudahili,"amesema Twaha.


from MPEKUZI

Comments