Mwanajeshi Anayedaiwa kuua askari mwenzake apandishwa kizimbani

Mwanajeshi MT 109795 Private Ramadhan Mlaku (28) amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shitaka la mauaji ya askari mwenzie, MT 79512 SGT Saimon Munyama.

Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo leo Jumatano Machi 14, 2018 saa tano asubuhi na gari la kubebea wagonjwa.

Alishushwa katika gari hilo akiwa juu ya kitanda cha wagonjwa na kupelekwa chumba cha mawakili wa Serikali ambapo alisomewa shtaka linalomkabili.

Akisomewa shtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakili wa Serikali, Mosii Kaima amesema mtuhumiwa huyo anadaiwa kufanya kosa hilo Oktoba 30, 2017.

Imedai kuwa mshtakiwa ambaye ni mwanajeshi wa kambi ya Jeshi Makongo siku hiyo akiwa Makao Mkuu ya JWTZ Upanga, Dar es Salaam alimuua askari mwenzie MT 79512 SGT Munyama.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa huyo hakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo.

Pia kosa hilo hakuna dhamana kwa mujibu wa sheria.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na Hakimu Simba aliutaka upande wa mashtaka kujitahidi kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo mapema.

Kesi imeahirishwa hadi Machi 28, 2018 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Baada ya kusomewa shtaka hilo mshtakiwa huyo alipandishwa tena katika gari la wagonjwa na kurudishwa mahabusu.


from MPEKUZI

Comments