Mbowe Atoa Waraka: Kuna Njama Kubwa Imepangwa Dhidi Yetu

Waraka Maalum wa Freeman Aikaeli Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai kwa Taifa

Leo tarehe 22 Machi 2018, mimi na viongozi wenzangu waandamizi wa Chadema tumetakiwa tena kuripoti Polisi.

Tunaokabiliwa na usumbufu huu ni pamoja na: Mhe Vincent Mashinji (Katibu Mkuu), Mhe. John John Mnyika, Mb na Naibu Katibu Mkuu Bara, Mhe. Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar; Mhe Halima J. Mdee, Mb, Mwenyekiti wa Bawacha, Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Mhe. John W. Heche, Mb, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti (Mara, Simiyu na Shinyanga) na Mjumbe wa Kamati Kuu; Mhe. Esther N. Matiko, Mb, Mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa Mara na Mweka hazina wa Bawacha Taifa.

Tuna taarifa pia ya kusudio la kumuunganisha Mhe. Peter Msigwa, Mb, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa (Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa) na Mjumbe wa Kamati Kuu katika shauri hili.

Historia ya wito:
Kwa muda wa wiki tano sasa, kufuatia sintofahamu kadhaa zilizojitokeza katika uchaguzi wa marudio wa Jimbo la Kinondoni, Dar es Salaam na Siha, Kilimanjaro, tumekuwa tukisumbuliwa kuripoti Polisi kila wiki kwa mashtaka ambayo hayajawahi kuwekwa bayana.

Katika kampeni na chaguzi hizi, palijitokeza mambo mengi ya ukiukwaji wa Haki za binadamu, ukiukwaji wa sheria za uchaguzi, matumizi mabaya ya madaraka ya kiserikali, udhalilishaji na unyanyapaa dhidi ya Vyama vya Upinzani, mauaji na mateso kwa viongozi wa vyama vya Upinzani na hata Wananchi wasio na hatia.

Wakati nenda rudi hii ikiendelea, tuna taarifa (asante teknolojia) kuwa zinapangwa njama mahususi za kutubambikia viongozi wa Chadema kesi za Mauaji au Uhaini ili kuhalalisha azma ya Watawala kutuweka mahabusu kwa muda mrefu, wakidhani kwa kufanya hivyo watakuwa wamefanikisha kufifisha na hata kuua kabisa uwepo wa Upinzani katika Taifa.

Jitihada hizo ni pamoja na kujaribu kuhusisha viongozi, wanachama na wapenzi wa chama chetu na tuhuma aidha za Kigaidi, Mauaji na hata Uhujumu wa Uchumi.

"Viongozi" hawa, wasaidizi na washirika wao wamejazana matumaini hewa kuwa vuguvugu la mabadiliko na uhitaji wa demokrasia ya kweli na vita dhidi ya udikteta katika taifa hili litazimwa kwa "kuwaficha, kuwapoteza na hata kuwaua" viongozi wa Chadema na wanaharakati wengine wanaoamini katika uhalisia huu.

Naam, njama hizi zaweza kuua baadhi, kujeruhi baadhi na hata kupoteza kadhaa! Lakini kamwe, hazitazima njozi za Watanzania wema kupigania haki na ustawi katika nchi yao.

Naamini kwa kuzima uongozi wa Chadema uliopo leo, siyo tu kutaruhusu kuchipua kwa kasi kwa uongozi mbadala, bali pia kutaamsha ari ya taifa kuongeza juhudi katika harakati ili hatimaye kutokomeza  uongozi wa kiimla katika nchi yetu.

Taifa lina msiba! Wanasiasa, wanaharakati, wanahabari na hata wasanii wanateswa, wanafungwa, wanajeruhiwa na wengine kuuwawa! Wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na nje wanalia! Viongozi wa dini wanachanganyikiwa! Wakulima, wafugaji na wavuvi wako hoi! Hata watoto na wanafunzi nao ni tishio kwa watawala!

Taifa limejazwa hofu. Wengi hawasemi, lakini wanataabika rohoni. Wanaisubiri fursa iwavyo vyovyote vile.

Nguvu, majeshi na silaha zao, magereza na mifumo kandamizi haziwezi kuwa suluhu ya uimla huu. Tuimarishwe badala ya kufifishwa.

Hatukimbii!! Tuko tayari kwa lolote, popote!

Shime Watanzania! Msitulilie! Lilieni watoto wenu na Taifa la kesho.

Na iwe vyovyote iwavyo! Damu, mateso, dhihaka dhidi ya maisha yetu iwe chachu ya dhati katika kutafuta Tanzania aliyoikusudia Mwenyezi Mungu yenye kusimamia haki, demokrasia, usawa, utu na ustawi kwa wote!!

Aluta Continua!!!
Freeman Aikaeli Mbowe


from MPEKUZI

Comments