Masogange augua siku ya kusomewa hukumu ya kesi inayomkabili

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kumsomea hukumu msanii Agnes Gerald maarufu kama Masogange anayekabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya kwa sababu anaumwa, amewekewa dripu na hawezi kutembea.

Hukumu hiyo ilitarajiwa kutolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri mara baada ya upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Costantine Kakula kuwaita mashahidi watatu kutoa ushahidi dhidi ya Masogange na kuufunga na mshtakiwa mwenyewe kujitetea.

Ilipofika saa 3:46 asubuhi leo Jumatano Machi 21, 2018 kesi hiyo iliitwa kwa Hakimu Mashauri na wakili wa Serikali, Adolf Mkini alieleza kuwa kesi ilipangwa kwa ajili ya hukumu ila mshtakiwa Masogange anayewakilishwa na wakili Ruben Simwanza hakuwapo.

Hata hivyo, mdhamini wa Masogange ambaye hakutaja jina lake alisimama na kuiambia mahakama kuwa Masogange hakufika mahakamani kwa sababu anaumwa na akawasilisha nakala za vyeti vya hospitali mahakamani hapo.

Mdhamini huyo amedai kuwa Masogange amewekewa dripu na hawezi hata kutembea.

Kutokana na hali hiyo Mkini ameiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya hukumu. Hukumu itasomwa Aprili 3, 2018. Wakili mwingine anayemtetea Masogange ni Nehemiah Nkoko.

Masogange wakati akijitetea katika kesi hiyo aliiomba mahakama imuachie huru kwa sababu hana kosa lolote.

Masogange  ambaye anakabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin na Oxazepam, katika utetezi wake amedai kuwa yeye hajawahi kutumia dawa za kulevya hata siku moja.

Akijitetea Masogange meidai kuwa mbali ya kuwa msanii pia alikuwa ni mfanyabiashara wa nguo.

Masogange katika kesi hiyo  anadaiwa kuwa kati ya Februari 7 na 14, 2017 katika maeneo yasiyojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam alitumia dawa za kulevya aina ya Heroin (Diacety Imophine).

Pia anadaiwa kuwa kati ya Februari 7 na 14, 2017 alitumia dawa za kulevya aina ya Oxazepam.


from MPEKUZI

Comments