Kamati ya Maadili TFF yamfungia Michael Wambura kujihusisha na soka maisha

Sekretariati ya Shirikisho la soka Tanzania TFF ilimfikisha Makamu wa Rais wa TFF Michael Wambura kwenye kamati ya maadili akikabiliwa na tuhuma tatu ikiwemo kupokea fedha za malipo TFF za malipo ambayo hayakuwa halali.

Jana mchana afisa habari wa TFF Clifford Mario Ndimbo aliwaambia waandishi wa habari kwamba Wambura amefanya makosa hayo huku akijua anashusha hadhi ya shirikisho hilo ikiwa ni kinyume na katiba ya TFF.

Ndimbo alisema  Wambura alikuwa na uhuru wa kufika mwenyewe mbele ya kamati na kutoa utetezi wake kwa njia mdomo, kutuma kwa maandishi au kupeleka mashahidi au kutuma mwakilishi ambaye ataambatana na barua ya uwakilishi. Wambura alituma mwakilishi ambaye ni Wakili Emanuel Muga kwa ajili ya kumtetea.

Alisema kamati hiyo iliyokaa jana ikiongozwa na Mwenyekiti wake Hamidu Ally Mbwezereni, wamemkuta na makosa matatu yatakayomfanya Wambura asijihusishe na masuala ya soka.

Kosa la kwanza amevunja kifungu no 73 kwa kupokea malipo yasiyo halali ya TFF, ambapo faini yake ni milioni 10, kutojihusisha na soka miaka mitano au maisha.

Kosa la pili kugushi malipo kwa jina la TFF enzi hizo (FAT), ambapo amezuiliwa kujihusisha na soka kwa miaka 5.

Kosa la tatu linalomkabili ni kushusha hadhi ya TFF, kosa ambalo adhabu yake iliyotolewa ni kutojihusisha na soka maisha.

Wakili wake, Emmanuel Muga amesema hakupewa nafasi ya kumtetea mteja wake kwa sababu kamati ilikuwa na dhamira yake ya kutaka kulimaliza suala hilo siku hiyohiyo (jana Machi 14, 2018).

“Ni kweli sikupewa nafasi ya kumtetea kwa sababu kamati ilikuja ikiwa na dhamira yake kutaka kulimaliza suala hilo siku hiyohiyo. Kwa hiyo nilivyowasilisha masuala ya kisheria ambayo ni ya kikanuni, kamati ilikataa ikasema sisi tunaamua tunavyoona”-Emanuel Muga, Wakili wa Wambura.



from MPEKUZI

Comments