Mwanamke achomwa moto na waganga wa jadi akitafuta uzazi

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, linawashikilia waganga wa jadi wawili ambapo mmoja ni mkazi wa Kijiji cha Obwere na Michael Jacob wa Omuga kwa tuhuma za kumjeruhi kwa kumuunguza moto, Emiliana Thomas anayeishi Kijiji cha Omuga wilayani Rorya.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Henry Mwaibambe alisema jana kuwa, majeruhi huyo ambaye ni mwanamke anayesumbuliwa na tatizo la kutopata ujauzito, waganga hao walimwaminisha kuwa ataupata.

Alisema walimwambia ili apate mtoto ni mpaka kuku imwagiwe mafuta ya taa na iteketezwe moto huku mama huyo akiwa ameishikilia mikononi.

Kamanda alisema baada ya waganga hao kuwasha moto ulimunguza na kumsababishia majeraha.

Mwaibambe alisema, awali waganga hao walimweleza mwanamke huyo kuwa anasumbuliwa na mashetani ndani ya tumbo na ndio yanayomfanya asizae.

Alisema walimweleza kwamba kuku ikiteketea ikiwa mikononi mwake atakuwa ameondokana na mashetani, hivyo ni lazima iteketezwe.

Kamanda huyo alisema baada ya waganga hao ‘kumsomesha’ mwanamke huyo alikubali na ndipo walipoimwagia mafuta ya taa kuku hiyo na kuwasha moto kwa kibiriti uliolipuka na kumjeruhi kifuani na mikononi.

Mwaibambe aliongeza kuwa, hali ya mama huyo ni mbaya na anaendelea na matibabu katika Hospital ya Kowak wilayani humo.

Mmoja wa waganga hao wa jadi, Jacob alisema tukio hilo ni ‘bahati mbaya’.

“Alikuja akiomba tiba, sasa kwa bahati mbaya mafuta yalikuwa yamemumwagikia mikononi na mikono ya nguo aliyokuwa amevaa ilikuwa hadi mikononi, wakati tumewasha moto ndipo ukamuunguza,” alisema Jacob.

Mwakilishi wa Chama cha Tiba Asili mkoani Mara, Jacob Matiko alilaani kitendo hicho kuwa hakiendani na taratibu za tiba na kinakiuka sheria inayozuia vitendo hivyo huku akiwataka waganga kutofanya utapeli iwapo hawawezi kufanya tiba kama matabibu asili.


from MPEKUZI

Comments