Waziri Mkuu Asema Serikali Haitasubiri Kuwaundia Tume Wezi na Mafisadi......Asisitiza kwamba atakayebainika atashughulikiwa hapo hapo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma nchini wasijihusishe na vitendo vya wizi, ufisadi kwani Serikali haitosubiri kuwaundia tume za kuwachunguza bali itawashughulikia hapo hapo.

Amesema Serikali haikotayari kuwavumilia watumishi wanaojihusisha na wizi, ubadhilifu, rushwa na uzembe, hivyo ni vema viongozi waliopewa dhamana wahakikishe wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Januari 15, 2018) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Musoma mkoani Mara akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku sita mkoani hapa.

“Fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo zinalenga kutatua kero za wananchi na si kuwanufaisha wachache wenye tamaa. Kama ni za ujenzi wa zahanati ijengwe na atakayezitafuna Serikali haitosita kumchukulia hatua.”

Waziri Mkuu asiwasisitiza watumishi wa umma kufanya kazi kwa mujibu wa sharia kwa sababu vitendo vya wizi, uzembe vinachangia kupunguza kasi ya kuwaletea maendelea maendeleo Watanzania.

Alisema lengo ni kuhakikisha azma ya Serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi hususan ni wale wa hali ya chini inatimia, hivyo aliwaagiza viongozi wa halmashauri wakiwemo Madiwani kusimamia vizuri miradi ya maendeleo.

Pia Waziri Mkuu aliwataka wakuu wa idara na watendaji wengine wa halmashauri kuacha tabia ya kukaa ofisini na dabala yake waende vijijini kwa ajili ya kuwafuata wananchi na kushirikiana nao katika kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.

Waziri Mkuu alisema watendaji hao wanatakiwa waachane na tabia ya kuwasubiri wananchi wawapelekee malalamiko yao kwa sababu baadhi yao hawana uwezo wa kufika katika ofisi zao.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


from MPEKUZI

Comments