Watuhumiwa wa ugaidi Arusha wavua nguo Mahakamani

Watuhumiwa katika kesi ya matukio mbalimbali ya ugaidi mkoani Arusha, Leo January 16, 2018 wamevua nguo na kubaki utupu wakati wakishushwa kwenye basi la Magereza la Kisongo walipofikishwa katika Mahakama ya hakimu mkazi Arusha.

Baadhi ya watuhumiwa wamefikia uamuzi huo wakidai kuchoshwa na hatua ya kufikishwa Mahakamani na kusomewa mashtaka kisha kurejeshwa mahabusu bila kesi yao kuanza kusikilizwa, jambo linalowalazimu kukaa mahabusu kwa zaidi ya miaka minne bila shauri lao kusikilizwa.

Mapema leo, mahabusu hao walifikishwa Mahakamani wakiwa kwenye  basi la magereza na kuamuriwa kuteremka, lakini baadhi yao waliteremka wakiwa hawana nguo na kutembea kuelekea zilipo mahabusu za Mahakama hiyo jambo lililowafanya wananchi waliokuwepo eneo la Mahakama kupata taharuki.

Kabla ya kufanya tukio hilo mahabusu hao wamekuwa wakilalamika katika Mahakama hiyo juu upelelezi kucheleweshwa katika shauri lao, wameiomba Mahakama imwamuru Mwanasheria wa Serikali kuharakisha upelelezi wa shauri lao kwa sababu limekuwa la muda mrefu na wao wakiendelea kuumia mahabusu.

Shauri hilo leo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na Hakimu Patricia Kisinda wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, ameahirisha shauri hilo kutokana na upelelezi kutokamilika hadi January 30, 2018.

Watuhumiwa hao wamerejeshwa mahabusu katika gereza kuu la Kisongo chini ya ulinzi mkali wa askari wa magereza.

April 25 mwaka jana baadhi ya mahabusu hao waligoma kushuka kwenye gari la Magereza jambo lililoilazimu Mahakama hiyo kuhamia nje na kuwasomea mashtaka na kisha kurejeshwa Mahabusu wakiwa chini ya ulinzi mkali.


from MPEKUZI

Comments