TAKUKURU Yamchukua Kaburu Ili Kumhoji Tena

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imemchukua Makamu wa Rais wa klabu ya Simba, Godfrey Nyange ‘Kaburu’ anayekabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha wa USD 300,000 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kumuhoji.

Mbali ya Kaburu, mshtakiwa mwingine ni Rais wa Klabu hiyo, Evans Aveva ambaye hakufika mahakamani hapo.

Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Leornad Swai amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa kwamba kesi hiyo haikupangwa leo isipokuwa wamemtoa Kaburu gerezani kwa kibali ili akahojiwe.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Nongwa alimkabidhi Kaburu kwa Wakili Swai huku akimtaka amrudishe leo kama alivyoomba, ambapo aliahirisha kesi hiyo hadi tarehe iliyopangwa January 25,2018.

Aveva na makamu wake, Geofrey wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha fedha USD 300,000.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15, 2016 wakionesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa USD 300,000 kwa Evans Aveva wakati si kweli.


from MPEKUZI

Comments