Serikali yatoa ufafanuzi Kuzuia matumizi fedha za kigeni

Serikali imesema haijazuia matumizi ya fedha za kigeni nchini bali imechukua hatua ya kudhibiti matumizi ya fedha hizo kulinda thamani ya shilingi ya Tanzania.

Kauli hiyo imetolewa leo Januari 15, 2018 na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alipokutana na wawakilishi wa wafanyabiashara mkoani Arusha kujadiliana mambo mbalimbali kwa ajili ya kukuza sekta ya biashara nchini.

Amesema sheria haijazuia matumizi ya fedha hizo nchini, inasisitiza kuwa watu wanapaswa kutambua kuwa sarafu ndiyo fedha halali kwa malipo ndani ya nchi.

“Tatizo kubwa tunalokumbana nalo ni uhuru ulioachiwa unaosababisha kushuka kwa thamani ya shilingi yetu. Kila mmoja anaweza kutumia fedha za kigeni, pia watumiaji wa fedha za kigeni hawafuati thamani ya fedha iliyoko sokoni. Kila mmoja anakuwa na kiwango tofauti cha thamani ya kubadili fedha,” amesema Dk Kijaji.

Amebainisha kuwa ili kuondoa changamoto hizo Serikali imeamua kurekebisha sheria ya matumizi ya fedha za kigeni na sheria ya Benki Kuu (BoT) ambayo inazitaka bei zote nchini zitangazwe kwa shilingi ya Tanzania.

Amesema bei hizo zinajumuisha kodi za nyumba za kuishi na ofisi, bei za ardhi, gharama za elimu na afya, bei za vyombo vya usafiri na vifaa vya kielektroniki.

“Bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja ambao sio wakazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni,” amesema na kuongeza,

“Hata hivyo kama mlengwa akitaka kulipa kwa shilingi ya Tanzania asilazimishwe kulipa kwa fedha za kigeni.”

Amezitaka vyombo vya dola kuchukua hatua za kisheria kwa wote watakaokiuka maagizo hayo yaliyotolewa na Serikali.


from MPEKUZI

Comments